Waziri Mkuu atoa agizo kwa Ma-RAS, Ma-DED

Muktasari:
- Waziri Mkuu ameitaka TOA wakahamasishe watu wajitokeze kwenye katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 2025
Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS) na Wakurugenzi (DED) nchini kumzungumzia mema Rais Samia Suluhu Hassan ili asitumie muda mwingi atakapopita kwenye maeneo yao wakati wa kampeni.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Aprili 14, 2025 alipozungumza na wajumbe wa mkutano wa 15 wa Taasisi ya Maboresho ya Mifumo ya Serikali za Mitaa (TOA).
Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jiji la Dodoma eneo la Mtumba ambako Majaliwa amesema ni muhimu watumishi hao wakamsemea mema Rais kwa kuwa, ndiye kiongozi wao.

Waziri Mkuu amewauliza watumishi hao kama wangetamani Rais Samia apate asilimia ngapi katika uchaguzi mkuu na zilisikika sauti wakisema apate asilimia 100.
Baadhi ya vyama vimekuwa vikilalamika kuhusu kuwatumia wakurugenzi kwenye usimamizi wa uchaguzi kwamba, huipendelea CCM.
"Sisi ni watumishi wa umma, Rais ndiye Rais wetu sasa kwa nini msimsemee, nataka mkafanye hivyo ili akifika kwa wananchi asalimie na kupita tu lakini kila kitu kiwe sawa," amesema Majaliwa.
Maagizo mengine Waziri Mkuu ameitaka TOA wakahamasishe watu wajitokeze kwenye katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 2025.
Nyingine ni kuwa makini katika maeneo wakati wa ukadiriaji wa makusanyo akidai baadhi hukadiria chini ili wakusanye zaidi na kuonekana wamefanya vizuri kwa malengo ya kupongezwa.
"Jifunzeni itifaki, kuna maeneo viongozi wanahisi kuwa mnawachukia kumbe ni kutojua itifaki, hilo ni somo muhimu sana kwenu," amesema.

Kwa upande mwingine amewaagiza wakurugenzi na makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha shule za sekondari za kata zinapata haki na kuzijengea uzio kwa kutumia mapato ya ndani.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewaagiza halmashauri zenye uwezo kutoa ajira za mikataba ili kupunguza kelele za uhaba wa watumishi.
Simbachawene amesema kuna maeneo halmashauri zinajiweza kiuchumi lakini inashangaza wanalalamika hawana watumishi.
Amewaagiza wakurugenzi kulipa madeni ya watumishi ambayo yameongeza ukilinganisha na mwaka juzi yalipokuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema amewataka watumishi kusimamia maadili na makusanyo ya fedha huku akisisitiza suala la uaminifu.
Mwisho