Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo sita yamsubiri Majaliwa bungeni

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kesho (Aprili 15, 2025), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwa na kibarua cha kujibu hoja zilizowasilishwa na wabunge, wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake, taasisi zake na Mfuko wa Bunge katika mwaka wa fedha  2025/2026.

Dodoma. Suala la wageni kupewa fursa ya kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, na changamoto ya ajira nchini, ni miongoni mwa hoja zitakazojibiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni jijini Dodoma kesho Jumanne, Aprili 15, 2025.

Hoja hizo mbili ni kati ya sita zilizoibuliwa na wabunge kuanzia Aprili 9, mwaka huu, katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/22026.

Sambamba na hizo, hoja nyingine ni utitiri wa mifuko ya uwezeshaji wananchi, kutoridhisha kwa usalama wa chakula, mradi wa Bonde la Mto Msimbazi, na kuangaliwa upya kwa mazingira ya ufanyaji biashara.

Pia, Majaliwa atakuwa na kibarua cha kujibu kuhusu mfumo wa elimu kutotengeneza wahitimu wenye weledi, na Serikali iondokane na utegemezi wa fedha za kuhudumia kwenye Virusi vya Ukimwi (VVU).

Majaliwa atajibu hoja hizo kesho (Aprili 15, 2025), wakati akihitimisha mjadala wa bajeti yake ya mwisho, aliyoomba kuidhinishiwa Sh782.08 bilioni kabla ya Tanzania kuingia katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.


Kazi kufanywa na wageni

Katika hoja ya ajira, wabunge walitaka Serikali iangalie upya suala hilo kwa kuongeza wigo wa maeneo ya kutoa ajira na kuondoa hali ya kujuana zinapotangazwa.

“Serikali ikitangaza nafasi za ajira, simu za wabunge zinaanza, watu wakiomba kusaidiwa kupata nafasi. Huu utaratibu wa utoaji ajira unatakiwa kuangaliwa upya,” amesema mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni.

Hoja hiyo ilipigiwa msumari na mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje, aliyesema suala la ajira bado ni changamoto kwa kuwa kuna wimbi la raia wa kigeni wanaochukua nafasi za wazawa.

Katika kuijenga hoja yake hiyo, Nusrat amesema wapo raia wa kigeni wanaouza hereni hadi za Sh3,000, hivyo Serikali iangalie upya mifumo kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama.

“Mheshimiwa Spika, kuna raia wa kigeni wanakopesha hadi bukubuku kama wanavyofanya Waha, nendeni mkaangalie,” amesema Hanje.

Mbunge wa Musoma Mjini, Vedatus Manyinyi, na Jesca Msambatavangu (Iringa Mjini), waliunga mkono hoja hiyo.


Mifuko ya uwezeshaji


Katika hoja yake, Neema amesema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwakwamua kiuchumi, lakini bado nia hiyo haionekani kwa waliopewa dhamana ya kusimamia.

“Hata sisi wabunge pia hatufahamu vizuri. Na kutokana na mikopo hii, nashauri iundwe tume itakayosaidia kuwezesha utoaji wa mikopo kwa wananchi,” amesema.


Mazingira ya biashara

Mbunge wa Bunda Mjini (CCM), Robert Chacha, amesema miaka 25 iliyopita ni tofauti na sasa, kwani mzazi alikuwa na uwezo wa kumpatia kijana wake Sh2 milioni kwa ajili ya kufanya biashara na akapata matokeo.

“Leo kitu hicho hakiwezekani kutokana na mambo mbalimbali na gharama zilizojitokeza na zinazowakabili wafanyabiashara. Ni vizuri Serikali ikatengeneza mpango maalumu wa kuweka uwiano wa kodi kwa wafanyabiashara,” amesema.

Chacha amesema kama kijana atapatiwa mkopo wa Sh1 milioni kama mtaji wa kuanzisha biashara, fedha hizo zote zitaishia katika gharama za uendeshaji kabla ya kufungua biashara husika.

Amesema mfanyabiashara huyo atalipa kodi na michango kabla ya kufungua biashara yake, na wakati huohuo masoko ya biashara yameingiliwa na wageni wengi wanaofika na mitaji mikubwa kuliko ya Watanzania.

Amesema hali hiyo itafanya kuwepo vijana waliokopeshwa na Serikali, lakini hawawezi kurejesha kwa sababu ya miundombinu iliyotengenezwa. Hivyo, lifanywe kila linalowezekana kuwalinda wafanyabiashara wadogo walioko nchini.

“Si kweli Watanzania hawataki kulipa kodi, lakini tunataka wale wanaosimamia katika vitengo vya kulipa kodi na wao wasaidie wafanyabiashara namna ya kulipa kodi katika usawa ambao unawaruhusu kuishi,” amesema, na kuungwa mkono na mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angeline Mabula.


Usalama wa chakula hauridhishi

Hoja ya kutoridhisha kwa usalama wa chakula, inayosababishwa na mwaka 2019 Serikali kufuta Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kisha kupeleka majukumu hayo kwa Shirika la Viwango la Tanzania (TBS), iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ni kibarua kingine kinachosubiriwa kujibiwa.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira, amesema TBS imeshindwa kuratibu na kudhibiti usalama wa chakula, na kwamba umefika wakati wapate kauli ya Serikali, kwa kuwa tangu mwaka 2021 wamekuwa wakiomba suala la udhibiti na usalama wa chakula lirejeshwe Wizara ya Afya.

“Huwezi kuendelea kuendesha suala la usalama wa chakula kibiashara. Suala la usalama wa chakula linahusu uhai wa Watanzania. Hatuwezi kuyaweka maisha ya Watanzania katika mazingira hayo kwa sababu ya kusimamia biashara,” amesema.


Fedha za Ukimwi

Kuhusu Serikali kuondokana na utegemezi wa fedha za kuhudumia kwenye Virusi vya Ukimwi (VVU), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilitaka Serikali kuja na mpango wa kuongeza fedha za ndani katika eneo hilo.

Kauli hiyo imekuja baada ya uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kupunguza msaada wa kibajeti katika fedha ambazo taifa hilo limekuwa likitoa kwa nchi, ikiwemo Tanzania.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2025/26, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jacqueline Kainja, amesema ni lazima Serikali ije na mpango wa kuongeza fedha za ndani katika eneo hilo.

Kwa upande wa Bonde la Mto Msimbazi lililopo jijini Dar es Salaam, ambalo limesababisha watu kupata mafuriko ya mara kwa mara, liliibuliwa na mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli.

Bonnah amesema bonde hilo linaendelea kuwapa shida wakazi wa Dar es Salaam kutokana na kupita katika majimbo mengine, ikiwemo Ilala.

“Juzi juzi mvua zimeanza kunyesha na watu wameendelea kupata mafuriko, na wananchi wanafahamu kuwa bonde liko katika mkakati wa kujengwa. Kwa hiyo tulikuwa tunataka katika majibu ya Waziri Mkuu atakapokuja, atuambie sasa wamefikia wapi?” amesema.

Baada ya Majaliwa kuhitimisha, itakuwa fursa kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), itakayowasilishwa na waziri wake, Mohamed Mchengerwa.Mwisho