Waziri Kijaji awanyooshea kidole askari wa Tawa
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Ashatu Kijaji (katikati) akikata utepe kama ishara ya kukabidhi vitendea kazi kwa mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori TAWA, ambayo ni magari manne yakiwemo matatu ya kufanyia doria za kidhibiti wanyama wakali na waharibifu, vilipizi na ndege nyuki alivyokadhi kwenye osifi ya TAWA mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Waziri wa Maliasili na Utalii, DK Ashatu Kijaji, ameikabidhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) vitendea kazi mbalimbali vya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu vyenye thamani ya zaidi Sh923 milioni.
Morogoro. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, ameonya tabia ya baadhi ya askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) kuwaomba wananchi wachangie mafuta ili waweze kufika katika maeneo yenye matukio ya uvamizi wa wanyama wakali na waharibifu.
Amesisitiza kuwa huduma hizo zinapaswa kutolewa bila kumtoza mwananchi gharama yoyote.
Dk Kijaji amesema hayo mjini Morogoro katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya zaidi ya Sh923 milioni kwa Tawa.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeongeza uwezo wa watumishi wa mamlaka hiyo kufika popote kwa kuwapatia pikipiki, magari pamoja na vifaa mbalimbali vya doria.
“Hatuna sababu ya kumwambia mtu hatuwezi kufika eti kwa sababu hatuna usafiri, mwananchi hatakiwi kuchangia mafuta, hawa watu tayari wameshavamiwa na wanyama wakali ama wanyama waharibifu sasa hiyo hela ya kukutumia watatoa wapi?” amehoji DK Kijaji.
Dk Kijaji amewataka askari wa Tawa kuwahudumia wananchi kwa heshima, utu na weledi, akisisitiza kuwa migongano kati ya binadamu na wanyamapori inapaswa kushughulikiwa kwa haraka.
Amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki bila usumbufu wowote.
Baadhi ya magari aliyokabidhi Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Ashatu Kijaji Kwa ofisi ya mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori TAWA mkoa wa Morogoro. Picha Hamida Shariff
“Huduma zetu tunazotoa kwa wananchi wetu lazima zizingatie utu wa watu wetu dhamira ya serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwatumikia wananchi wetu kwa utu, heshima na haki, hivyo migongano kati ya binadamu na wanyamapori ishughulikiwe kwa haraka, tumia uadilifu na weledi wako kuwahudumia wananchi wetu," amesisitiza DK Kijaji.
Vifaa vilivyokabidhiwa na Waziri Kijaji kwa Tawa vinajumuisha magari manne, ndege nyuki, vilipuzi pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kufukuza wanyama wakali wanapovamia mashamba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tawa, Meja Jenerali Hamisi Semfuko, amesema bodi imeandaa mkakati mpya wa ukusanyaji wa mapato unaotarajiwa kuiwezesha Tawa kukusanya Sh187 bilioni kufikia mwaka 2027/2028 kupitia ubunifu na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Tawa, Mlage Kabange, amewataka wananchi wanaoishi maeneo yenye uwepo wa wanyama wakali kufuata maelekezo ya wataalamu na kuepuka kufanya shughuli zao usiku.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kupunguza madhara yanayotokana na wanyama hao.