Waziri Gwajima ashauri Siku ya Wanaume itambuliwe rasmi nchini

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dk Dorothy Gwajima akizungumza kwenye kongamano la siku ya wanawake kwa Kanda ya Ziwa lililofanyika wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Muktasari:
- Amesema kutambuliwa kwa siku hiyo kutapunguza ukatili wa kijinsia kwakuwa wanaume watakuwa sehemu ya suluhisho kwa kushiriki majadiliano na kampeni zinazolenga kumaliza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na makundi mengine.
Bukombe. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amesema ipo haja ya Siku ya Wanaume Duniani, inayoadhimishwa Novemba 19 ya kila mwaka, kutambuliwa rasmi nchini kama inavyoadhimishwa Siku ya Wanawake, ili wanaume watambua nafasi yao katika kulinda na kuendeleza familia sambamba na kupinga ukatili kwenye jamii.
Akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Kanda ya Ziwa, lililofanyika leo Jumapili, Machi 2, 2025, wilayani Bukombe, mkoani Geita, Dk Gwajima amesema kutambua siku hiyo kutatoa nafasi kwa wanaume kushiriki kikamilifu katika mijadala kuhusu haki za kijinsia, malezi bora na ustawi wa familia.
Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Machi 8, 2025, ambapo kitaifa yatafanyika mkoani Arusha, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika maelezo yake, Dk Gwajima amesema, “Hatuwezi kuendelea mbele kama wanaume hawajaelewa dhana ya usawa wa kijinsia, kwani wao ni wababa. Ni muhimu waongee na watoto wao wa kike na wa kiume kuhusu masuala haya.”
Amesema tayari sera mpya ya maendeleo ya jinsia na wanawake ya mwaka 2023 imewajumuisha wanaume, baada ya kubaini kuwa wanawake hawawezi kuendelea mbele kama wanaume hawajaielewa dhana hiyo na kwenda kuzungumza na wanawake.
Amesema kutambuliwa kwa siku hiyo kutapunguza ukatili wa kijinsia, kwani wanaume watakuwa sehemu ya suluhisho kwa kushiriki majadiliano na kampeni zinazolenga kumaliza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na makundi mengine.
Kupitia siku hiyo, wanaume watakumbushwa jukumu lao la msingi katika malezi na makuzi ya watoto, hivyo kuchangia jamii yenye maadili bora.

“Wanawake huwa tunakutana na kujadili mambo yetu, kama wanaume siku yao itakuwa jukwaa la kuimarisha mshikamano kati ya wanaume na wanawake katika kupambana na changamoto za kijamii kwa pamoja,” amesema.
Akisoma risala ya wanawake wa Kanda ya Ziwa, mwakilishi wa wanawake hao, Salome Cherehani, amesema wanawake wanaunga mkono jitihada za Rais Samia katika uanzishwaji wa majukwaa ya wananchi kiuchumi, ili waweze kuwa na lengo moja la kupata fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo mikopo isiyo na riba na ile ya riba nafuu.
Amesema uwepo wa fursa ya madini umewezesha wanawake kujipatia kipato, kujiimarisha kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.
Cherehani amesema, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini wanakutana na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kuchimbia, hali inayowafanya kuingia ubia na wanaume, na matokeo yake hupata mapato kidogo.
Amesema, pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu katika sekta ya afya, bado ipo changamoto ya upungufu wa wataalamu wa afya, hali inayochangia vifo visivyo vya lazima kwa wanawake na watoto wachanga.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema hadi sasa Sh1.5 bilioni zimetolewa na halmashauri za Geita kwenye vikundi 173, ambapo kati ya hivyo, vikundi 63 ni vya wanawake.
Katika sekta ya madini, vikundi 60 vya wanawake vimepatiwa leseni, na amesema mwanamke ana nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa familia, kwani ndiye mlezi na mwalimu wa kwanza kwenye familia.
Baadhi ya wanawake walioshiriki kongamano hilo wameunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuadhimisha Siku ya Wanaume, wakisema wanawake wanapokaa na kujadili bila kuwashirikisha wanaume, juhudi hizo hazizai matunda, kwani wahusika wakuu wa ukatili dhidi ya wanawake ni wanaume.
“Ni vema Serikali imeona jambo hili kuwa lina umuhimu ili wao nao wawe na ajenda yao. Tukiwa na ajenda moja, tutaweza kushirikiana kutokomeza ukatili wa kijinsia. Jambo hili liwe la vitendo, lisiwe limesemwa tu na kuachwa,” amesema Jazaah Komba.