Wazee washtukia vijana kudai urithi bado wakiwa hai

Muktasari:
Wilaya ya Kahama inakadiriwa kuwa na wazee 6, 792 ambapo asilimia 50 wanaishi maeneo ya vijijini wakijishughulisha na kilimo na ufugaji.
Kahama. Wazee wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wamesema watoto wao kudai urithi wakati wao wakiwa hai ni chanzo cha unyanyasaji na mauaji dhidi yao.
Takwimu zinaonyesha wazee 22 wamepoteza maisha katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2017 katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya imani ya ushirikina.
Wazee hao wamezungumza Juni 27, 2023 kwenye kikao cha wazee kilichofanyika wilayani humo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya kuondokana na migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha baadhi yao kukatwa mapanga na wengine kudhurumiwa mali zao.
Baadhi ya wazee, Samwel Bundala na Victoria Thomas wamesema wenzao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na watoto wao wakiwalazimisha kutoa urithi badala wao kutafuta mali zao.
“Tunaiomba Serikali itusaidie sisi wazee maana tuna fanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii kwa kutuhumiwa kujihusisha na ushirikina na wengine wanakatwa mapanga,”amesema Victoria
Akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu wa Baraza la wazee Taifa, Anderson Lyimo amekemea vitendo vya unyanyasaji wa wazee unaofanywa na baadhi ya watu kwenye jamii na ngazi ya familia na kutoa rai kulilinda kundi hilo.
Amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kukomesha vitendo vya ukatili kwa wazee na kuiomba jamii kuunga mkono jitihada hizo kwa kupaza sauti zao kulaani vitendo hivyo.
Ofisa Ardhi mteule Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Yusuph Luhuma amewashauri wazee umuhimu wa kupima maeneo yao na kuwa na mipaka ya kudumu badala ya kutumia mipaka ya miti ambayo haiwezi kudumu.
Amesema mipaka ya kudumu itasaidia kuepusha migogoro ya uvamizi wa mipaka na kuwawezesha wazee kuwa na maeneo yao yaliyopimwa watakayoyatumia kufanya shughuli za maendeleo.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Julias Chagama amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wazee ili kuvikomesha.
Amesema kutokana na elimu kuifikia jamii imesaidia mauaji ya wazee kupungua tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo yalikuwa yakiripotiwa mara kwa mara lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa.