Wazee wa ‘Tuma kwa namba hii’ watinga kortini

Wakazi 12 wa Sumbawanga mkoani Rukwa, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 50 yakiwemo ya kujipatia Sh 9.2milioni kwa njia ya udanganyifu . Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Vijana 12 kutoka Sumbawanga mkoani Rukwa wame wanakabiliwa na mashtaka 50 yakiweno ya kutakatisha fedha, kujipatia fedha, kutuma ujumbe ‘Tuma pesa kwa namba hii’.
Dar es Salaam. Vijana 12 kutoka Sumbawanga mkoani Rukwa, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa wakikabiliwa na mashtaka 50 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kutuma ujumbe wakishawishi kuwa wao ni waganga wa kienyeji, kutakatisha fedha pamoja na kujipatia fedha Sh9.2 milioni kwa kutuma ujumbe usemao ‘Tuma pesa kwa namba hii’.
Washtakiwa hao ni Pius Mahali (29), Best Sinyangwe (24) ambaye ni dereva bodaboda, Andrea Kipeta(31), Lusekelo Jimmy(32) maarufu kama Mkondya; Michael Kanyegele (28) na Lucas Mpanduzi(19).
Wengine ni Steven Selemani (18), Emanuel Kawimbe (30), Alvin Mbingi (30), Charles Kachoma (20) maarufu kama Kachoma, Fabian Mwananyali (18) na dereva bodaboda, Alex Tung’ombe (27).
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo, leo Jumatano Juni 5, 2024 na kusomewa mashtaka yao, ikiwa imepita wiki moja, tangu wakazi 12 wa Ifakara mkoani Morogoro walipofikishwa mahakamani hapo, wakikabiliwa na mashtaka 32, wakijipatia Sh10 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Washtakiwa hao wamesomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 15,200/ 2024 na Wakili wa Serikali, Erick Kamala akishirikiana na Aaron Titus mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya.
Kati ya mashtaka 50 yanayowakabili washtakiwa hao; mashtaka 19 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, 17 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, 12 ya kutuma ujumbe mfupi wa maandishi wenye ushawishi wakijifanya wao ni waganga wa jadi, shtaka moja la kutakatisha fedha na lingine ni kuongoza genge la uhalifu.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Mbuya amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Pia shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Akiwasomea mashtaka yao, wakili Kamala amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Septemba Mosi, 2023 na Mei 5, 2024 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walianzisha mtandao wa uhalifu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wenye kushawishi watu mbalimbali na kujipatia Sh9.2milioni.
Katika shitaka la pili linalomkabili Mahali peke yake, anadaiwa Desemba 19, 2023 alituma ujumbe yenye ushawishi uliosomeka “Mjukuu wangu nimekusaidia sanaa mpaka sasa una majumba, magari ya kifahari lakini hata kuja kunishukuru nizirudishe mali kwenye mizimu? Basi nakutakia utajiri mwema.”
Shtaka la tatu linamkabili Sinyangwe peke, anadaiwa Mei 6, 2024 eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mshtakiwa alituma ujumbe wenye ushawishi uliosomeka “Leo unakufa majini yamekasirika sana,” kwa kutumia namba iliyosajiliwa kwa jina la Samwel Kikwembe.
Pia, Sinyangwe anadaiwa kutuma ujumbe iliosomeka “Binti kuna shida inaenda kukutokea leo muda huu wa jioni.”
Kwa upande wake mshtakiwa Kipeta anadaiwa Februari 6, 2024 maeneo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mshtakiwa alituma jumbe ukisomeka “666 jiunge na chama huru cha Freemason Tanzania umiliki mali pesa majumba mvuto vipaji pete bila kafala kwa kujiunga piga namba hiyo.”
Shtaka sita linamkabili Jimmy ambaye anadaiwa January 9, 2024 alituma ujumbe uliosomeka, “mzee Tadeo mganga anatibu kisukari, uzazi kifafa dawa ya pesa mapenzi guvu za kiume kurudisha mme au mke, kesi, kuvuta wateja zindiko nyota tiba mbalimbali mpigie kwa namba hiyo.”
Katika mashtaka ya saba yanayomkabili Donati ilidaiwa Januari 22, 2024 alituma ujumbe “Ile dawa ya kusafisha nyota yako na zindiko la mali zako tayari nimekamilisha mjukuu wangu uje uchukue nashukulu pia kama dagu imeaza kufanya kazi.”
Kwa upande wake Mpanduzi, naye anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka, “mjukuu wa Kisile naona biashara ya mabasi sasa inatosha umashanunua mabasi mengi, sasa uje tena Sumbawanga nikupe dawa ya kusafisha nyota na ya ndagu mimi ni babu yako wa Sumbawanga mzee Ramadhani.”
Mshtakiwan Selemani yeye anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka, “Mpigie Mzee Said kwa mwenye uhitaji wa mali, nyota biashara, kurudisha mke na magonjwa sugu.”
Shtaka la 10 na 11 linamkabili Kawimbe ambapo anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka, “Kaka nashukuru sana kwa mtaalamu uliyeniletea, kwani kwa sasa baba kapona kabisa. Na ajabu leo asubuhi tumekuta wale wezi walioiba vile vitu getini wakiwa wamevibeba vyote sasa nakuomba sana tena kwa ustazi kamwambie kuwa nimpe nini kama zawadi? Pls jibu.”
Vile vile, washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kujipatia fedha Sh9.2 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa watu tofauti wakidanganya kuwa wao ni waganga wa kienyeji.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Septemba Mosi 2023 na Mei 5, 2024 ndani ya wilaya ya Sumbawanga na maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Katika shtaka la kutakatisha fedha, linalowakabili washtakiwa wote, wanadaiwa katika kipindi hicho na maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitakatisha Sh9.2 milioni wakati wakijua wazi kuwa fedha hizo hizo zinatokana na makosa tangulizi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mbuya ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 27, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili, kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.