Prime
Watuhumiwa walikamatwa kwa mganga wa jadi-Shahidi

Katika gazeti letu la jana, tulikuletea ushahidi wa shahidi wa tisa wa Jamhuri, Mkaguzi wa Polisi, Samwel Mwaimu ambaye ndiye alikuwa mkuu wa timu ya operesheni iliyokuwa na jukumu la kukamata watuhumiwa wa mauaji.
Tuliishia timu hiyo ambayo ilikuwa ni moja kati ya timu tatu zilizoundwa kufuatilia mauaji hayo ilivyomkamata Jalila Zuberi ambaye ni mshitakiwa wa nne na namna walivyompeleka polisi jijini Arusha.
Leo tutakuletea mwendelezo wa namna timu hiyo ilivyoendelea kupokea taarifa kutoka timu ya intelijensia na ile ya mitandao iliyokuwa inafuatilia mawasiliano ya simu na namba ilivyoweza kukamata watuhumiwa wa mauaji.
Shahidi huyo wa tisa wa Jamhuri, aliendelea kueleza kuwa wakiwa jijini Arusha, walipewa majina mengine mawili ya watu waliotakiwa kukamatwa wilayani Kaliua Mkoa wa Tabora ambao ni Karim Issa Kihundwa na Sadick Mohamed Jabir.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa kwa mganga wa jadi katika Kijiji cha Limbuli, Kaliua na katika mahojiano, Karim Kihundwa alikiri kufanya mauaji hayo na kueleza bunduki (SMG) alikuwa ameiacha Moshi.
“Nilimuuliza hiyo SMG iko wapi akasema aliihifadhi Wilaya ya Hai katika Kijiji cha Golotu. Aliniambia pia kama tukimpata kaka yake aitwaye Said Mohamed, yeye ndiye anajua ni wapi bunduki hiyo imefichwa,” alidai Mwaimu ambaye ni shahidi.
“Baada ya kuniambia hivyo, mara moja niliwasiliana na RCO (mkuu wa upelelezi mkoa) kwa simu na kumpa taarifa na baada ya muda RCO alimpigia na kumjulisha kuwa wamefanikiwa kuipata hiyo silaha. Baada ya hapo tuliwapeleka Kituo cha Polisi Kaliua.
“Lakini wakati ule nafanya mawasiliano na RCO, mtuhumiwa mwenzake Sadick Mohamed Jabir alikuwa kwenye gari na Konstebo Selemani akaja kuniambia hata Sadick naye amemwambia amekiri kuhusika katika mauaji hayo,” alidai Mwaimu.
Wakiwa Kituo cha Polisi cha Kaliua, aliandika maelezo ya mshtakiwa Karim Kihundwa ambaye alikiri kuwa yeye ndiye alitumia SMG kumuua Bilionea Msuya, hivyo akaiomba Mahakama ipokee maelezo yake kama kielelezo.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Majura Magafu walipinga kupokewa maelezo hayo, pingamizi lililokubaliwa na Jaji Maghimbi aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, huku akiwalaumu polisi kwa kufanya makosa.
Akitoa uamuzi, Jaji Maghimbi alisema kwa ushahidi wa Inspekta Maimu, inaonyesha mshitakiwa alitoa ushirikiano na kuhoji ilikuwaje polisi wachukue saa nne kufika Kituo cha Polisi cha Kaliua, ambacho kipo mkoani Tabora.
Jaji Maghimbi alisema Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, inataka maelezo ya mtuhumiwa yaandikwe ndani ya saa nne tangu kukamatwa kwake, lakini hayo yaliandikwa saa tano baadaye.
Baada ya kutupwa kwa maelezo hayo muhimu kwa upande wa mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdalah Chavula aliendelea kumuongoza shahidi kutoa ushahidi kama ifuatavyo:
Wakili Chavula: Hebu ieleze Mahakama, Septemba 13, 2013 wakati ukizungumza na Karim (mshitakiwa wa tano) alipokueleza uhusika wake, aliweza kukueleza alivyohusika na tukio hili?
Shahidi: Alinieleza kuwa yeye ndiye aliyekamata bunduki na ndiye aliyemfyatulia risasi Erasto Msuya.
Wakili Chavula: Siku iliyofuata baada ya kuwa umeshamhoji, nini kilifuata?
Shahidi: Baada ya kumhoji tuliondoka kwa ajili ya kumleta Kilimanjaro.
Wakili Chavula: Nini kilijiri mlipofika Kilimanjaro?
Shahidi: Tulimpeleka kwa RCO na alikiri tena kwamba alishiriki na ndiye aliyeshika bunduki.
Wakili Chavula: Aliyasemea wapi na nani alikuwapo?
Shahidi: Aliyasema hayo mbele ya RCO Ramadhan Ng’anzi na mimi pia nilikuwepo.
Wakili Chavula: Baada ya kusema maneno hayo, nini kilifuata?
Shahidi: RCO alitoa maelekezo tumpeleke kwa mlinzi wa amani.
Wakili Chavula: Kule Tabora mnasema mliwakamata watu wawili, yule mwingine anaitwa nani?
Shahidi: Anaitwa Sadick Jabir (mshitakiwa wa sita).
Wakili Chavula: Kule Tabora kijijini wakati unamhoji Kihundwa, Jabir alikuwa wapi?
Shahidi: Alikuwa kwenye gari.
Wakili Chavula: Eneo gani?
Shahidi: Kijiji cha Limbula.
Wakili Chavula: Yeye naye alipelekwa wapi mlipotoka kijijini?
Shahidi: Naye tulikuja naye hadi kituo cha Polisi Kaliua akawekwa mahabusu.
Wakili Chavula: Nini kilitokea?
Shahidi: Na yeye aliwekwa mahabusu hadi Septemba 14, 2013.
Wakili Chavula: Nini kilitokea siku hiyo?
Shahidi: Jabir alisema aliacha vitu vyake kijijini Limbula tulienda naye hadi kijijini.
Wakili: Baada ya kufika kijijini mlikuta hiyo mizigo yake na pesa?
Shahidi: Sikuona hizo pesa akipewa.
Wakili Chavula: Nini kiliendelea?
Shahidi: Baada ya kutoka Limbula tulirudi naye katika Kituo cha Polisi Kaliua.
Wakili Chavula: Nini kikaendelea?
Shahidi: Kilichoendelea ni kuandika maelezo yao.
Wakili Chavula: Nani aliandika maelezo ya Sadick (Jabir)?
Shahidi: Ni Koplo Seleman.
Wakili Chavula: Hebu tueleze, mlipofika Moshi nini kilitokea kwa Sadick?
Shahidi: Naye tulimpeleka kwa RCO na alikiri kuhusika katika mipango ya kumuua Msuya.
Wakili Chavula: Hebu tuambie, alieleza uhusika wake ulikuwa vipi?
Shahidi: Alisema yeye alipigiwa simu na rafiki yake aitwaye Mredii (Shaibu Jumanne) alimwambia kuna kazi, yeye atafute mtu wa pili wa kufanya naye hiyo kazi. Alipomuuliza ni kazi gani alimwambia kuna kazi ya kumuua mtu itafanyikia Arusha. Alimtafuta rafiki yake anaitwa Karim (Kihundwa) na waliondoka naye kwenda Arusha kwa mtu anaitwa Sharifu (Mohamed, mshitakiwa wa kwanza).
Siku hiyo ya tukio yeye alikuwa na pikipiki moja na Mredii, kazi yao ilikuwa kusaidia kama kungetokea dharura.
Alisema siku hiyo alienda eneo la tukio akaegesha pikipiki mbali kidogo akiangalia tukio zima likifanyika na baada ya kukamilika aliondoka na pikipiki.
Wakili Chavula: Shahidi, alikueleza alielekea wapi?
Shahidi: Alielekea Sanyajuu.
(Maelezo hayo yalimnyanyua Wakili Majura na kupinga shahidi huyo kueleza maelezo aliyodai ni ya ungamo ya mshitakiwa huyo wa sita, wakati hakuna maelezo ya mshitakiwa huyo yaliyokuwa yapokewa kama kielelezo).
“Maelezo ya ungamo linalodaiwa kuwa la mshitakiwa wa sita hayajapokewa mahakamani kama kielelezo. Shahidi anataka kuingiza ungamo hilo kwa mlango wa nyuma. Tumevumilia sana tukidhani maelezo ya mshitakiwa wa sita yataletwa,”
Wakili Magafu alisema kisheria, Koplo Seleman ndiye alipaswa kuleta kortini maelezo hayo ya ungamo la mshitakiwa wa sita hata kama ni maelezo ya mdomo anayodaiwa kutamka na kuomba ushahidi huo uondolewe.
“Kwa hiyo tunaiomba Mahakama, ushahidi wote alioutoa shahidi huyu kuhusu oral confession (ungamo la mdomo) la Sadick uondolewe kwenye kumbukumbu za Mahakama,” alisisitiza wakili Magafu
Akijibu hoja za pingamizi hilo, alisema shahidi huyo ni sahihi kwa sababu anasema alikuwepo kwa RCO na alikisikia kwa masikio yake kile alichokuwa akikitolea ushahidi mahakamani.
Wakili Chavula alisema ushahidi wanaoutoa unashabihiana na kusema swali lilipo ni je, mshitakiwa ndiye aliyemuua marehemu? Na kwamba hilo ndilo ambalo Mahakama inatafuta majawabu.
“Shahidi wetu anasema mshitakiwa ndiye aliyemuua marehemu na Mahakama iko hapa kutafuta nani aliua, kwa hiyo ushahidi wake ni relevant (una mahusiano)” alisisitiza wakili Chavula.
Akitoa uamuzi mdogo juu ya mabishano hayo ya kisheria, Jaji Maghimbi alisema kimsingi upande wa mashitaka unatumia vibaya mchakato wa ushahidi huo wa mdomo wa mshitakiwa.
“Kwa vile RCO alitoa ushahidi wake hapa mahakamani, alikuwa na nafasi nzuri ya kuishawishi mahakama kuwa mshitakiwa alikiri mbele yake wakati akimhoji kwa mdomo,” alisema Jaji.
Kutokana na hilo, Jaji Maghimbi alisema ushahidi wote wa Inspekta Maimu unaozungumzia kuwa mshitakiwa wa sita alikiri mbele ya RCO unaondolewa katika kumbukumbu za Mahakama.
Uamuzi huo wa Jaji ulionekana kuwakanganya mawakili wa Serikali. Wakili Chavula aliomba ahirisho la nusu saa ili waweze kushauriana namna ya kuendelea na shahidi huyo.
Baada ya ahirisho hilo, wakili Chavula, Wakili Mwandamizi Omary Kibwana na mawakili Kassim Nassir na Lucy Kyusa, waliondoka eneo la Mahakama na kwenda ofisini kushauriana.
Usikose kufuatilia simulizi ya kesi hii ya mauaji ya Bilionea Msuya kesho