Watu watano mbaroni wakidaiwa kukutwa na tani 1.8 za bangi

Muktasari:
- Watuhumiwa walikamatwa maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam, katika operesheni iliyofanyika Agosti 28 hadi Septemba 2, 2024.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watuhumiwa watano wakidaiwa kukutwa na bangi aina skanka akiwamo Richard Mwanri (47) aliyekuwa akitafutwa kwa madai ya kujihusisha na biashara hiyo.
Mwanri anatuhumiwa kuwa mpokeaji wa dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali kuziingiza nchini na usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazama maeneo mbalimbali.
Mfanyabiashara huyo anayedaiwa kuwa na mtandao mkubwa wa dawa za kulevya amekamatwa na wenzake wakiwa skanka kilogramu 1,815.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 10, 2024 jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema watuhumiwa walikamatwa maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam, katika operesheni iliyofanyika Agosti 28 hadi Septemba 2, 2024.
"Richard (47) ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde Wilaya ya Kinondoni, wengine tuliowakamata ni Felista Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguruni Wilaya ya Ubungo na mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo.
“Mtuhumiwa mwingine ni Athumani Mohammed (58) mfanyabiashara na mkazi wa Tanga, Omary Mohamed (32) ambaye ni Dereva bajaji mkazi wa Buza Dar es Salaam, pia yupo Juma Chapa (36) mkazi wa Kiwalani na katika operesheni hiyo gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T551CAB na bajaji namba za usajili MC844CZV zilikamatwa," amesema.
Kamishna Lyimo amesema hivi karibuni wamekuwa wakikamata dawa za kulevya aina ya skanka maeneo mbalimbali nchini huku akisema mamlaka hiyo inafanyia uchunguzi utengenezaji wa dawa hiyo.
"Tayari tumeanza uchunguzi wa kubaini kemikali zinazowekwa kwenye skanka, kemikali zinazowekwa kwenye dawa hizi ni kwa ajili ya kutengeneza urahibu na kumfanya mtu asiache, tunafanya utafiti na tutatoa taarifa," amesema.
Fahamu kuhusu skanka
Skanka ni bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) inayoweza kuharibu mfumo wa fahamu na akili pamoja na kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama moyo, figo na inni.
Matumizi ya skanka kwa wajawazito husababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni ikiwamo kuathiri maendeleo ya ubongo na mtoto kuzaliwa na uzito pungufu.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya duniani iliyotolewa Vienne nchini Australia Juni 2024, maeneo yaliyohalalisha matumizi ya bangi, uzalishaji wa bidhaa za bangi zenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC uliongezeja.
Kamishna Lyimo akidokeza hilo, amesema katika nchi hizo kumekuwa na ongezeko la watu wanaohitaji tiba kutokana na matumizi ya bangi na kuongezeka kwa watu wenye matatizo ya akili.