Watu 16,000 walivyotazama ‘Live’ mahubiri ya Askofu Gwajima

Muktasari:
Wakati Askofu Gwajima anaanza kuongea hadi kufikia saa 7:20 mchana, idadi ya watazamaji ilikuwa imefikia 16,000 na baada ya Askofu kumaliza kuongea, ndipo idadi ilianza kushuka kutoka 16,000 hadi 12,000 hadi kufikia 10,000.
Dar es Salaam. Ama kweli Askofu Josephat Gwajima ni kiboko, ni maneno unaweza kuyatumia kuelezea namna watazamaji 16,000 walivyojitokeza kusikiliza mbashara (Live), mahubiri yake ya leo Jumapili Juni mosi, 2025 jijini Dar es Salaam.
Idadi hiyo ni ya wale tu waliokuwa wakitizama ‘Live’ muda ambao Askofu Gwajima alizungumza kupitia runinga ya Rudisha TV, idadi inayotarajiwa kuongezeka kadri kiu ya kusikiliza na kurudia mahubiri hayo itakavyoongezeka.
Ingawa idadi hiyo ya watazamaji inaweza kuonekana kubwa katika siku za karibuni, lakini haijavunja rekodi ya mwaka 2017 alipokuwa na mgogoro na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda sasa mkuu wa mkoa Arusha.
Mathalan mwaka 2017, Februari 9 TV hiyo ilipata watazamaji wa ‘live’ 90,000, Februari 26 ( 83,000), Machi 12 (132,000), Machi 19 (354,000) na Juni 4 ilipata 316,000.
Katika mahubiri yake ambayo wengi walitarajia atawajibu wabunge waliomshambulia baada ya kuzungumza suala la utekaji, jana alieleza kuwa anaamini chama chake (CCM) hakikubali utekaji na hakina sera ya utekaji.
Tangazo la kwamba Askofu Gwajima angeongea Live lilianza kuonekana katika TV hiyo saa 5:30 asubuhi likiwa na kichwa “Bishop Gwajima anaongea,” hapo ndipo idadi ya watazamaji ilianza kupanda ghafla na kufikia 1,200 ilipofika saa 6:00.
Saa 6:15, matangazo ya Live yalifunguka na kulianza kwaya ikitumbuizwa kwa lengo la kuandaa waumini na watazamaji kuwa Askofu angeingia na ilipofika saa 6:48 mchana, Askofu Gwajima aliingia kanisani hapo akishangiliwa na waumini.
Wakati Askofu Gwajima anaanza kuongea hadi kufikia saa 7:20 mchana, idadi ya watazamaji ilikuwa imefikia 16,000 na baada ya Askofu kumaliza kuongea, ndipo idadi ilianza kushuka kutoka 16,000 hadi 12,000 hadi kufikia 10,000.
Katika mahubiri yake, Askofu Gwajima alielezea namna anavyokerwa na matukio ya utekaji na kutoa orodha aliyonayo ya watu 80 na kwamba idadi imeongezeka na kumtaja Sheikh mmoja huko Zanzibar aliyedaiwa kutekwa na baadaye kuuawa.
Askofu Gwajima alisema genge hilo la utekaji halichagui wa kumteka, kwani kuna mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM huko Mwanza ametekwa na hajulikani alipo na siku za karibuni alitekwa kada wa Chadema huko Mbeya, Mdude Nyagali.