Watoto watatu wa familia moja wateketea kwa moto Rombo
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa.
Muktasari:
- Watoto watatu wa familia moja ambao walikuwa wamelala chumba kimoja wameteketea kwa moto katika kijiji cha Samanga, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kuungua moto.
Rombo. Watoto watatu wa familia moja waliokuwa wamelala chumba kimoja wameteketea kwa moto katika kijiji cha Samanga, Kata ya Kirongo Samanga, wilayani hapa, mkoani Kilimanjaro baada ya nyumba waliyokuwa wamelala kuungua moto.
Watoto hao waliteketea kwa moto alfajiri ya kuamkia leo Jumamosi, Desemba 16, 2023 wakati wazazi wao wakiwa wametoka kwenda kwenye utafutaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na waliofariki dunia ni Oseline Laswai (9) mwanafunzi wa darasa la nne, Jolin Laswai (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza, waliokuwa wakisoma Shule ya Msingi Baraka pamoja na mdogo wao Anna Laswai (3).
"Leo iliungua moto nyumba iliyojengwa kwa mbao na kusababisha vifo vya watoto watatu ambao ni wakazi wa kijiji cha Samanga.
"Wakati tukio linatokea wazazi wa watoto hawa walikuwa wamekwishatoka kuelekea kwenye shughuli zao za kujipatia kipato majira ya saa 10:00 alfajiri," amesema Kamanda Maigwa.
Kamanda Maigwa amesema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa na miili ya watoto hao imehifadhiwa katika kituo cha afya Karume.