Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watoto wa mitaani wafichua sababu kutorudi chini ya malezi ya familia

Mtoto Othman Deo akisoma risala kwa niaba ya watoto wenzake

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa takwimu  za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jumla ya watoto 8,372 wanaoishi na kufanya kazi mtaani wameokolewa na kupatiwa huduma mbalimbali katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025.

Arusha. Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wameelezea ugumu wanaokabiliana nao katika kuishi chini ya uangalizi wa wazazi au walezi  baada ya kuokolewa kutoka mitaani.

Wamesema kuwa kauli za kukatisha tamaa, vitendo vya unyanyapaa, ukatili wa vipigo, ushawishi wa makundi rika, dawa za kulevya imekuwa kikwazo cha baadhi yao kurudi tena chini ya uangalizi wa wazazi au walezi wanapookolewa mitaani.

Kwa mujibu wa takwimu  za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jumla ya watoto 8,372 wanaoishi na kufanya kazi mtaani wameokolewa na kupatiwa huduma mbalimbali katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025.

Aidha 1,056 kati ya hao wapo katika makao ya watoto na nyumba salama, 86 wapo kwa walezi wa kuaminika na wengine bila kutaja idadi wanadaiwa kuunganishwa na familia zao.

Akizungumza mbele ya watoto na wadau wa maendeleo ya jamii, leo Aprili 14, 2025,  Mtoto Othman Deo (14) amesema kuwa wanashukuru Serikali na baadhi ya mashirika na taasisi mbalimbali zinazojitolea kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, lakini baadhi yao wanashindwa kurudi chini ya malezi kutokana na changamoto mbalimbali.

Mtoto Deo ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mitaani iliyoanza Aprili 12, 2025 chini ya kauli mbiu ‘imarisha ushirikiano kuzuia watoto kuishi mitaani’.

Maadhimisho hayo kimkoa yaliyoandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na Kituo cha ‘Amani Center’ yalikusanya wadau na watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kupata chakula cha pamoja na kubadilishana changamoto na utatuzi.

“Baadhi ya watoto mitaani wamekuwa wakiokolewa nikiwemo mimi lakini tunashindwa kumudu kuishi tena chini ya malezi kutokana na kuitwa  majina ya unyanyapaa, lakini pia vipigo na manyanyaso ukizingatia wengine tumeshaathirika kisaikolojia juu ya matukio tuliyopitia mitaani” amesema.

Erick John (16) amesema baadhi ya changamoto wanazopitia mitaani ni ukosefu wa chakula, mavazi na malazi pia matibabu kwa wakati, na zaidi kupigwa mara kwa mara na watu wakionekana kama wezi huku baadhi yao wakitumia vitu vya kulevya ili kujiondoa katika msongo wa mawazo.

Amesema changamoto nyingine ni kunyanyaswa kingono na kijinsia lakini pia kubakwa na kulawitiwa mara kwa mara na wenzao ambao ni wakubwa au wana jamii inayowazunguka.

“Kikubwa tunaomba Serikali itambue tuna haki ya kupendwa, kulindwa na kuheshimiwa maana hata sisi tuna haki ya kuishi, unakuta mwenzenu kafanyiwa kitendo kibaya ukienda polisi hawakusikilizi au unapoumwa ukienda hospitali hawakutibu” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kuwawezesha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kujikwamua kiuchumi wanapoonesha nia ya kutaka kusoma fani mbalimbali, au mitaji ya biashara pia wapate huduma muhimu za afya wanapougua bila vikwazo.

Ofisa Tawala wa Wilaya ya Arusha, Malack Tateni ameiomba jamii kila mmoja kutimiza wajibu wake katika malezi ili kupunguza idadi ya watoto wanaoishi mitaani.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuondoa wimbi la watoto wa mitaani, hivyo kuwataka wazazi kurudi katika msingi wa malezi ili kuepuka watoto wapya lakini pia kuwalea vema wanaorudishwa kwa ndugu zao ili wasirudi tena mitaani.

“Jamani hakuna mtoto wa mtaani hapa maana hakuna mtaa unaozaa, hawa wote wamezaliwa na wazazi lakini kutokana na changamoto kadhaa zimewafikisha hapa basi tuwasaidie kuepuka kadhia wanazokumbana nazo.”

“Watoto wamesema hapa wanakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo za kubakwa, kulawitiwa, kupigwa, kufanya biashara haramu na kukosa fursa ya kupata elimu na wengine kupoteza maisha,  hivyo tuone bado tunao wajibu wa kumsaidia mtoto huyu sio kutekeleza ukatili huo kwao” amesema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Dennis Mgiye amesema kwa jiji la Arusha pekee kuna zaidi ya watoto 544 wanaoishi na kufanya kazi mitaani, huku zaidi ya asilimia 90 wakitoka nje ya jiji hilo.