Wateja watelekeza Sh2.9 bil benki

Dar es Salaam. Wakati watu wengi wanatamani kupata pesa ili kukidhi mahitaji mbalimbali, kuna wengine wanabembelezwa wakazichukue, lakini wamegoma.
Hali hii inatokana na kile kilichoelezwa na Bodi ya Bima ya Amana nchini (DIB) kwamba kuna Sh2.9 bilioni za waliokuwa wateja wa benki mbalimbali zilizofungwa hazijachukuliwa, licha ya kutoa taarifa mara kwa mara.
Hata hivyo, kiasi hicho ni kile kilichopo kwenye kinga ya amana ambapo mpaka Februari mwaka huu ilikuwa ni kwa amana zisizozidi Sh1.5 milioni.
DIB wanasema tangu mwaka 2000 hadi Juni mwaka huu, jumla ya benki tisa ziliwekwa kwenye mufilisi lakini ni asilimia 75 pekee ya wenye amana wamechukua amana zao.
Benki hizo tisa ni Greenland Bank Tanzania Limited (2000), Delphis Bank Tanzania Limited (2003), FBME Bank Limited (2017), Mbinga Community Bank Plc (2017), Njombe Community Bank Limited (2018) na Meru Community.
Nyingine ni Bank Limited (2018), Covenant Bank for Women (T) Limited (2018), Kagera Farmers' Cooperative Bank Limited (2018) na Efatha Bank Limited (2018).
Mkurugenzi Mtendaji wa DIB, Isack Kihwili alisema fedha hizo zipo na wenye amana wanaweza kuzichukua muda wowote kupitia benki ya biashara ya TCB.
“Jumla ya wateja ambao amana zao zilikuwa katika kinga ya DIB ni 58,036 wakiwa na thamani ya Sh11.97 bilioni, lakini mpaka Septemba 22, mwaka huu amana zilizochukuliwa ni asilimia 75.03 huku watu 36,355 wakiwa hawachukua fedha zao ambazo ni wastani wa zaidi ya Sh82,000 kila mtu," alisema Kihwili.
Hata hivyo, Kihwili alisema sehemu kubwa ya wenye amana ambao hawajafuata amana zao za akiba yao benki ilikuwa chini ya Sh20,000 huku wachache ndiyo walikuwa na zaidi ya Sh20,000 hadi Sh1.5 milioni.
“Kuna kawaida ya watu kupuuzia kufuatilia kiwango kidogo cha pesa, lakini wapo ambao sababu zao ni zaidi ya kiwango chao kuwa kidogo. Wapo wanaodai fedha nyingi, lakini hawajazifuatilia kwa sababu zao wenyewe,” alisema Kihwili ambaye aliongeza kuwa matangazo yamekuwa yakifanyika kuwataarifu.
Asema sheria iko kimya juu ya hatima ya fedha hizo zisipochukuliwa, hivyo wanachokifanya sasa wanazizungusha ili zizalishe na kulinda thamani yake akitolea mfano wa ununuzi wa hati fungani za Serikali na maeneo mengine ambayo ni salama kwa uwekezaji.
Respisius Daniel ambaye alikuwa na akaunti katika benki ya Kagera Famers alisema, “akaunti yangu nilikuwa naitumia kupokelea fedha za mauzo ya kahawa, zikiingia nilikuwa nazitoa sidhani kama nina pesa inayozidi Sh40,000 huko hivyo sioni umuhimu wa kuihangaikia.”
Hata hivyo, mmoja wa watumishi wa moja ya benki ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alieleza kuwa wateja wengi wanaamini ipo siku benki hiyo itafufuka na kuendeleza amana zao.
Hata hivyo, Mhasibu Mwandamizi wa DIB, Romuli Mtui akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika mwishoni mwa wiki alieleza kuwa taratibu za BoT haziruhusu ufunguaji wa benki iliyowekwa kwenye mufilisi kwa sababu yoyote ile hivyo wasiochukua amana zao wakidhani ipo siku benki yao itarudi wanasubiri muujiza ambao hautotimia.
Takwimu za DIB zinaonyesha kuwa wateja katika benki hiyo waliokuwa kwenye amana walikuwa wanadai Sh1.48 bilioni lakini mpaka sasa zimechukulia Sh1.04 bilioni na kiasi ambacho hakijachukuliwa ni Sh437.3 milioni.