Watatu mbaroni shambulizi la wanafunzi Uganda

Wananchi nchini Uganda wakizika moja ya miili ya wanafunzi waliouawa katika shambulizi mwishoni mwa wiki iliyopita nchini humo.

Muktasari:

  • Polisi nchini Uganda wamewatia watu watatu mbaroni kufuatia shambulizi la wanafunzi wiki iliyopitia nchini Uganda.

Uganda. Mamlaka ya Uganda imesema kuwa imewakamata watu watatu ikiwahusisha na shambulio dhidi ya wanafunzi Ijumaa mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo takribani watu 40 waliuawa.

Waathiriwa wengi walikuwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Lhubiria iliyoko katika mji wa Magharibi wa Mpondwe, ambapo wanafunzi walichomwa moto hadi kufa katika bweni lao.

Mkuu wa Wilaya eneo lililoathiriwa, Joe Walusimbi amesema kukamatwa kwa watu hao ni kutokana na taarifa za wakazi wa eneo hilo.

Walusimbi aliongeza kuwa Jeshi la Uganda bado linawatafuta wanamgambo hao wa Kiislamu ambao wamekuwa wakilaumiwa kwa shambulio hilo na wanaripotiwa kukimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shambulio dhidi ya shule hiyo ni tukio la kwanza la aina hiyo ndani ya Uganda kwa miaka mingi ambapo kundi la waasi la ADF ndio linaloshutumiwa kutekeleza shambulio hilo.

Mnamo 1998, waasi wa ADF walishambulia Taasisi ya Kiufundi ya Kichwamba wilayani Kabarole na kuwachoma moto wanafunzi 80 hadi kufa na kuwateka nyara zaidi ya 100 nchini humo.

Kundi la ADF liliundwa Mashariki mwa Uganda katika miaka ya 1990 na kuanza vuguvugu dhidi ya Rais wa muda mrefu, Yoweri Museveni, kwa madai ya mateso ya serikali dhidi ya Waislamu.

Baada ya kushindwa na jeshi la Uganda mwaka 2001, ilihamia Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC.

Mwanzilishi mkuu wa kundi hilo, Jamil Makulu, alikamatwa nchini Tanzania mwaka 2015 na yuko kizuizini katika gereza la Uganda.

Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha shughuli zao kutoka ndani ya DRC kwa miongo miwili iliyopita.