Watatu kizimbani wakituhumiwa kughushi, kukwepa kodi Sh171 milioni
Watuhumiwa wa ukwepaji kodi na uhujumu uchumi, Batholomeo Philipo (Kushoto mwenye ndala) na Bernado Wandela (Kulia)mmiliki wa Kiwanda cha Makha Beverage Company Limited, wakifikishwa katika mahakama ya Hakimu mkazi Geita.
Muktasari:
- Makosa wanayotuhumiwa nayo ni kughushi stempu za kielektroniki kinyume cha sheria, ukwepaji kodi pamoja na kuisababishia hasara Serikali.
Geita. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, watuhumiwa watatu kwa makosa manne likiwamo la uhujumu uchumi na kukwepa kodi zaidi ya Sh170 milioni.
Waliofikishwa mahakamani katika shauri hilo namba 11236/2026 ni Bernado Wandela (Mkurugenzi wa kiwanda cha Makha Beverage Company Limited), Batholomeo Philipo ‘Shauri’ ambaye ni mkemia na mshtakiwa wa tatu ni kiwanda cha Makha Beverage Company Limited.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 14, 2026 katika Mtaa wa Magogo ‘A’, Manispaa ya Geita ambapo walikutwa na boksi 451 za pombe kali aina ya Doz M Vodka zikiwa na stempu za kughushi na kukwepa kodi ya Sh171,516,454.
Watuhumiwa hao wamepandishwa kizimbani leo Ijumaa Mei 21, 2026 na kusomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Jaines Kihwelo akisaidiana na Auni Chilamula mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cleofas Waane.
Akizungumza na waandishi wa habari, Wakili wa Serikali, Auni Chilamula ameyataja makosa yanayowakabili kuwa ni kukutwa na bidhaa zilizowekwa stempu za kughushi ambayo ni kinyume na kanuni ya 36(1)(i) ya kanuni ya stempu za kielektroniki ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho ya kanuni ya 3(e) ya marekebisho ya kanuni za stempu za kielektroniki ya mwaka 2024.
Kosa la pili ni kukwepa kodi kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 95(1)(d) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438 Marejeo ya 2023. Kosa la tatu ni kuisababishia Serikali hasara kinyume na aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza ikisomwa pamoja na (57)(1) na 61(2) ya makosa ya uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya 2023.
Watuhumiwa wa ukwepaji kodi na uhujumu uchumi,Batholomeo Philipo(Kushoto mwenye ndala) na Bernado Wandela(Kulia)mmiliki wa Kiwanda cha Makha Beverage Company Limited,wakifikishwa katika mahakama ya Hakimu mkazi Geita.
Aidha, kosa la nne ni utakatishaji fedha ambayo ni kinyume na kifungu cha 12(d) na 13(1)(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Sura ya 12 iliyofanyiwa marekebisho 2023.