Watanzania hawali nyama na kunywa maziwa inavyotakiwa

Muktasari:
- Serikali imesema licha uzalishaji wa vyakula yakiwemo maziwa na nyama, bado ulaji uko chini kulinganisha na viwango vya kimataifa.
Moshi. Katibu wa wizara ya Mifugo na uvuvi, Rashid Tamatama, amesema kuwa ulaji wa nyama na unywaji wa maziwa nchini bado uko chini na imekuwa changamoto kubwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP).
Amesema mujibu wa takwimu za shirika hilo, mtu hutakiwa kula nyama kilogramu 50 kwa mwaka na maziwa lita 200, lakini Watanzania hula kilogramu 15 za nyama na lita 50 za maziwa kwa mwaka.
Akizungumza leo Oktoba 12,2021 kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya chakula duniani ambapo Kitaifa yatafanyika Mkoa wa Kilimanjaro, Tamatama amesema kuna haja ya serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuhakikisha kiwango cha ulaji wa nyama na maziwa kinafikia viwango vya kimataifa.
Soma hapa:Unywaji wa maziwa washuka nchini
Amesema pia ulaji wa samaki na mayai bado kiwango kiko chini huku uzalishaji ukiwa juu, akisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya ‘Zingatia uzalishaji na mazingira endelevu kwa lishe na maisha bora’ imelenga kuhamasiaha ulaji huo.
"Ulaji wa vyakula vya protini na wanga bado uko chini, licha ya kuwepo kwa mikoa hapa nchini ambayo inazalisha kwa wingi," amesema Tamatama.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel, amesema mikoa ambayo ndio inazalisha kwa wingi vyakula vya aina zote hapa nchini ndio yenye utapiamlo.
"Mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Songwe inaongoza kwa uzalishaji wa vyakula vya wana na protini laiki ni mikoa ambayo inaongoza kwa lishe duni," amesema Mollel.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai, amesema ulaji wa vyakula lishe kama unywaji wa maziwa pamoja na ulaji wa samaki, mayai na nyama upo chini, Hivyo kuwataka wananchi kutumia vyakula hivyo kwa wingi.