Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wa afya zaidi ya 450 kuweka kambi Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda (aliyevaa nguo nyeupe) akikagua maandalizi ya kambi ya siku saba ya madaktari bingwa na wataalam wa afya zaidi ya 450, itakayoanza Juni 24,2024 katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid. Kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Charles Mkombachepa.

Muktasari:

  • Kambi hiyo ya siku saba itaongozwa na madaktari bingwa na watoa huduma za afya zaidi ya 450 kutoka kwenye hospitali na taasisi za kifaya za kitaifa na kikanda,  lengo likiwa ni kutoa huduma ya vipimo, matibabu na dawa bure.

Arusha. Madaktari bingwa na watoa huduma za afya zadi ya 450 kutoka hospitali na taasisi za afya nchini, wanatarajia kutoa huduma ya vipimo na matibabu bure katika kambi maalumu ya siku saba mkoani Arusha.

Kambi hiyo inatarajiwa kuwa na madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, watatoa huduma za vipimo, matibabu na dawa bure ikiwemo magonjwa ya moyo, figo, shinikizo la damu, saratani, kinywa na meno, macho, afya ya akili na magonjwa mengine.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Juni 22, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua maandalizi ya kambi hiyo itakayofanyika katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.

Amesema kambi hiyo itaanza Jumatatu Juni 24, 2024 hadi Juni 30, 2024 katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid ambapo kwa sasa maandalizi mbalimbali yanaendelea uwanjani hapo ambapo kunatengenezwa katika mfumo wa hospitali, mahema yakiwa yamewekwa kuzunguka uwanja mzima.

Amesema wataalamu hao wanatoka katika hospitali za kitaifa, kikanda na mikoa na kuwa hadi sasa hospitali na taasisi zaidi ya 28 zimethibitisha ushiriki wake.

“Lengo kuu la kambi hii ni kumuwezesha kila mwananchi kupata huduma bora ya kibingwa. Wote tunajua kwamba matibabu ni gharama na vipato havifanani, kwenye suala la afya kuna watu wameuza nyumba zao, kuna watu wameuza viwanja.

“Kuna watu wamefilisika biashara wakipambana kuwauguza ndugu zao na kama mnakumbuka nyakati nyingine watu wameshindwa hata kukomboa miili ya ndugu zao, sababu ya kuwa na madeni kutokana na uwezo mdogo au umasikini wa kulipia gharama za matibabu,” ameongeza.

Ametaja hospitali hizo ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati Benjamin Mkapa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Nyingine ni Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Mt Meru, Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Mirembe, Hospitali ya Aga Khan na nyingine za Serikali na binafsi kutoka maeneo mbalimbali nchini..

Makonda amesema shughuli hiyo itakuwa endelevu ili lijenge utamaduni wa wananchi kupima afya zao na kuwa hata ikitokea mtu akabainika anatakiwa kufanyiwa upasuaji, ataenda kufanyiwa bure katika hospitali zilizopo mkoani hapa na kuwa kipaumbele ni kwa kina mama wajawazito, wazee na watoto.

“Uwanja unatengenezwa katika mfumo wa hospitali kuanzia unapoingia unasajiliwa, unapelekwa eneo husika kama utahitaji kipimo utafanyiwa, kipimo utafanyiwa maabara ambazo zitakuwepo hapa na majibu yakipatikana utapewa dawa,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkombachepa amewataka wakazi wa Arusha kutumia fursa hiyo kikamilifu ikiwemo wanaume kujitokeza kwa wingi.

“Tunaamini madaktari wa mkoa wa Arusha watapata ujuzi kutoka kwa wataalamu wanaotoka hospitali hizo nyingine na niwasihi wanaume kujitokeza kwa wingi. Miongoni mwa magonjwa tutakayotoa tiba ni tezi dume na kwa sasa kipimo chake kimeboreshwa, siyo cha zamani walichokuwa wanakwepa watu wengi,” amesema.