Wataalam watoa ‘nondo’ za mafanikio kwa wanawake wajasiriamali, waajiriwa

Baadhi ya wanawake wanachama wa kikundi cha Kibondo Women Gala cha Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wakifurahia jambo wakati wa kikao chao kilicholenga kujijengea uwezo wa kiutendaji na uwajibikaji kwa familia na jamii.
Muktasari:
Pamoja na kujiheshimu katika mahusiano na ndoa zao, wanawake pia wameshauri kufanya kazi kwa bidii katika eneo la uzalishaji mali kuwezesha mchango wao katika maendeleo ya familia na jamii kuonekana wazi, badala ya kujibweteka na kuwa tegemezi kwa wanaume.
Kibondo. Wanawake walio kwenye mahusisnao na ndoa wametakiwa kuwaheshimu na kushirikiana na wenzao wao katika majukumu yote ya kijamii na kifamilia kama njia ya kuepuka migogoro ambayo baadhi huishia kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia.
Pamoja na kujiheshimu katika mahusiano na ndoa zao, wanawake pia wameshauri kufanya kazi kwa bidii katika eneo la uzalishaji mali kuwezesha mchango wao katika maendeleo ya familia na jamii kuonekana wazi, badala ya kujibweteka na kuwa tegemezi kwa wanaume.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wanawake wanachama wa kikundi cha Kibondo Women Gala cha Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Mtaalam wa masuala ya Saikolojia, Epsalia Malya amesema tabia ya kujibweteka na uvivu kwa baadhi ya wanawake husababisha wapuuzwe na kutothaminiwa ndani ya familia na jamii kwa ujumla.
‘’Wanawake ni lazima tubadilike kifikra na kimtazamo kwa kuchapa kazi kwa bidii katika maeneo yote ya uzalishaji mali; kamwe tusichague kazi wala kukalia kujipamba. Kila mwanamke ajiepushe na tabia ya uvivu kwa kufanya kazi kwa bidii kuongeza pato la familia,’’ amesema Epsalia
Amesema wanawake walioajiriwa wafanye kazi kwa bidii, weledi na ubunifu; walioko kwenye sekta ya biashara na ujasiriamali nao wafanye vivyo hivyo ili hatimaye mchango wao uonekane katika familia na jamii yao.
Mtaalam mwingine wa Saikolojia, Sadaka Gandi amesema wanawake kutambua na kutumia vema nafasi na nguvu yao ya ushawishi kwenye masuala ya uzalishaji mali siyo tu kutamaliza tatizo la kiuchumi, bali pia vitedo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia vinavyotokana na umaskini.
‘’Changamoto nyingi zinazikabili jamii, hasa wanawake zinatokana na kutojitambua na kutojituma kwa wanawake walioko kwenye ndoa au mahusiano. Wanawake tubadilike kwa kila mmoja kujitambua, kujituma na kumheshimu mwenza wake,’’ amesema Gandi
Doreen Lyimo, Mwenyekiti wa Kibondo Women Gala chenye lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji wanawake wajasiriamali na waajiriwa katika sekta binafsi na umma amesema matunda ya umoja huo tayari yameanza kuonekana baada ya wanachama wake kuongeza bidii na tija katika shughuli zao.
‘’Pamoja na elimu kwa wanawake ya kufanya kazi kwa bidii kulingana na mazingira yao ya kazi, wanachama wetu pia wanajengewa uwezo kumudu malezi na majukumu ya kifamilia,’’ amesema Doreen
Amesema pamoja na kujengewa uwezo kiutendaji, wanachama wa kikundi hicho wanaofanya vizuri katika maeneo yao ya ujasiriamali, afya, elimu na ustawi pia hupewa tuzo maalum kutambua mchango wao kwa jamii kama sehemu ya motisha.