Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasiojulikana wamuua kikatili mgambo maarufu mjini Moshi

Muktasari:

  • Mwili wa marehemu umepatikana alfajiri leo Jumatano  Februari 21, 2024 katika eneo la uwanja wa Mandela katika kata hiyo ya Bomambuzi ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake na ukilazwa katika dimbwi la damu.

Moshi. Mgambo mashuhuri katika kata ya Bomambuzi Manipaa ya Moshi ambaye pia alikuwa dereva bajaji, farjala Abdallah ameuawa kikatili na watu wasiojulikana, huku Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro likiahidi kuwasaka kwa udi na uvumba waliofanya mauaji hayo.

Mwili wa Abdallah  umepatikana alfajiri ya leo Februari 21,2024 katika eneo la uwanja wa Mandela ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake na umetelekezwa  katika dimbwi la damu.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi, Azizi Kalokola akizungumza eneo la tukio, amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo.

"Kufuatana na vyanzo tulivyonavyo na wataalamu tulio nao, uchunguzi hautachukua muda kama mtatoa ushirikiano, tunaomba mtupe taarifa," amesema Kalokola.

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na eneo ulikokutwa mwili huo, wamedai usiku wa manane walisikia mtu akisema asiuawe yeye siyo mwizi, lakini hawakujua nini kilichokuwa kikiendelea.

"Usiku saa 7:37, nilisikia sauti, jamani msiniue mimi siyo mwizi, sasa hatukuelewa ni upande upi na sikujua kilichoendelea mpaka anapiga kelele na ni kina nani walikuwa wanampiga na ni kwa sababu gani," amesema Hamis Idd mkazi wa eneo hilo.

Naye Abubakari Kilema amesema alifika eneo la tukio saa 12:30 asubuhi na kuukuta mwili ukiwa na majeraha huku eneo la pembeni likiwa na damu nyingi hali inayoonyesha ndipo palipofanyikia mauaji.

"Baada ya kufika eneo la tukio, tuliona eneo ambalo inaonekana marehemu alipigwa kwa muda mrefu, hatujui ni nini kilitokea na kina nani waliohusika na tukio hili, tunawaachia Polisi waendelee na uchunguzi kuwabaini wahusika," amesema. 

“Kifo hiki kimetuumiza sana, marehemu alikuwa anafanya shughuli zake hakuwa na shida na mtu.”

"Marehemu alikuwa katibu wa madereva wa bajaji,  alikuwa akifanya kazi za mgambo kata na dereva bajaji, hakuwa na shida na mtu, na jana nilikuwa naye sasa sijui nini kilitokea, tumeumia sana," amesema  Zena Kidashari ambaye ni ndugu wa Abdallah.

Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu amewataka wananchi kutoa ushirikiano kuwezesha kupatikana kwa wahusika wa tukio hilo, huku akitangaza kutoa kitita cha  Sh500,000 kwa mtu atakayetoa taarifa fiche na sahihi zitakazosaidia kukamatwa kwa watu waliofanya mauaji hayo.