Waomba kuchangiwa ujenzi kituo cha afya

Muktasari:
- Wadau waombwa kuchangia ujenzi kituo cha Afya kilichojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuokoa maisha ya wajawazito na watoto.
Songwe. Mbunge Vwawa mkoani hapa, Japhet Hasunga ameungana na wananchi wa kitongoji cha Isangu Kata ya Hasanga kuomba wadau kuchangia kukamilisha ujenzi wa Kituo cha afya kitakacho hudumia wananchi 12,000 ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi .
Kata hiyo ambayo inahudumia vitongoji vitano imeelezwa kuwa tangu nchi ipate uhuru hakujawahi kuwepo na kituo cha afya wala hosptali ya mtu binafsi hali inayosababisha wanawake wajawazito kujifungulia njiani.
Mbunge Hasunga ametoa ombi hilo leo Alhamisi Oktoba 6, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isangu mara baada ya kupokea mabati 288 yenye thamani ya Sh 10 Milioni kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB).
“Baada ya wananchi kukubaliana kuanza ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kimefikia hatua ya kupaua niliongea na watu wa Benki kuomba watuchangie mabati na leo yamepokelewa kwa ajili ya kuendelea na Ujenzi,” amesema.
Amesema kuwa mbali na kupokea mabati bado kuna mahitaji mbalimbali ili kuweza kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi hususan wakina mama wajawazito ambao wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma.
Mkazi wa Kijiji cha Isangu, Lyidia Swebe amesema kuwa kukosekana kwa huduma za afya katika kata hiyo ni changamoto kubwa inayochochea hata watoto wadogo kushindwa kupata chanjo zinazotolewa na Serikali za kukabiliana na magonjwa.
“Huku tunategemea zaidi kupata matibabu katika hosptali ya Mbozi Mission au ya Wilaya ambapo kuna umbali mrefu na ukihitaji usafiri wa pikipiki unagharimu kati ya Sh5,000 mpaka 10,000 ambapo kwa wananchi kwenye kipato cha chini wanashindwa kumudu,” amesema.
Meneja wa Kanda wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Saimon Mlelwa amesema wamelazimika kuchangia mabati kutokana na umuhimu wa kituo hicho cha afya kwa wananchi hususan upatikanaji wa huduma ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
“Tulipokea maombi kutoka kwa Mbunge na tulifika kujionea kama benki tuna utaratibu wetu kuchangia katika Sekta ya elimu na afya ikiwa ni sehemu ya faida kwa kila mwaka,” amesema.
Diwani wa Kata ya Hasanga, Mirick Nzowa amesema kuwa ukosefu wa kituo cha afya ni changamoto hata kwa jamii kwani inapotokea dharula wanalazimika kutumia gharama kubwa za usafiri hali ambayo inawataathiri wananchi wa kipato cha chini.
“Kata hii hiki ni kituo cha kwanza kujengwa kwa nguvu za wananchi ambapo mpaka kufikia hatua ya kupaua kimetumia Sh 11 Milioni kati ya hizo Sh 8 Million ni nguvu za wananchi na endapo kikikamilika kitahudumia wakazi 12,000 na punguza msongamano wa wagonjwaa katika hosptali ya Wilaya,” amesema.