Wanawake Stamico wahamasisha matumizi ya nishati rafiki Briquetts

Baadhi ya watumishi wa Stamico wakiwa kwenye maandamano ya kusherehekea siku ya Wanawake dujiani Machi 8, 2025 katika Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salam.
Muktasari:
- Stamico imeamua kupeleka nishati rafiki ya briquettes kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika kitaifa Arusha ili kuonesha kwa vitendo jinsi inavyotumika kwa namna tofauti kulingana na uhitaji.
Dar es Salaam. Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limesema litaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kuwa na watu wengi wanaotumia nishati hiyo.
Lengo ni kuwawezesha wanawake na wasichana kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Msimamo huo umetolewa na Ofisa Rasilimaliwatu Mwandamizi wa Stamico, Leah Jericho kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2025 yaliyofanyika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Leah amesema Stamico imeamua kupeleka nishati rafiki ya briquettes kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Arusha ili kuonesha kwa vitendo jinsi inavyotumika kwa namna tofauti kulingana na uhitaji.
"Nitoe hamasa kwa wanawake nchini hasa wale wanaotumia nishati chafu za kuni na mkaa unaotokana na miti kuchangamkia nishati hiyo inayopatikana kwa bei nafuu," amesisitiza Leah.
Matumizi ya nishati safi yana umuhimu mkubwa, Desemba 2, 2023 wakati wa uzinduzi wa mradi wa Nishati Safi Afrika, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza namna wanawake wanavyoathirika na nishati safi.
"Wanawake wanaathirika kiafya wakati wa kupika kwa kuni na mkaa, watoto wa kike wanapoteza muda mwingi kutafuta kuni, hivyo kukosa muda wa kutosha katika masomo. Karibu asilimia 80 ya mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, hutumia nishati chafuzi," amesema
Pia, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2023 ikionyesha idadi ya watu bilioni 2.4 duniani, sawa na robo ya watu wake, hutegemea nishati chafuzi kwa ajili ya kupikia, jambo ambalo limesababisha hekta milioni 3.9 za misitu, kupotea kila mwaka barani Afrika.
Ripoti hiyo inafanunua kuwa, kutokana na matumizi ya nishati chafu ikiwamo kuni na mkaa, watu milioni 6.7 hufariki dunia kila mwaka duniani, kutokana na uzalishaji wa hewa chafu wakiwamo watu milioni 3.2 wanaopoteza maisha kutokana na hewa chafu inayozalishwa katika kaya kwa njia za kuni na mkaa.
Inaeleza kuwa, bila kuwa na utekelezaji wa sera thabiti, watu bilioni 2.1 wanakadiriwa kuendelea kukosa huduma ya nishati safi na teknolojia ifikapo mwaka 2030.