Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaougua kifafa walia na unyanyapaa, huduma

Mwenyekiti wa Uwakita, Dk Saidi Kuganda akizungumxa hii leo Agosti 8, 2024 kwenye kikao cha wadau wa ugonjwa wa Kifafa kilichofanyikia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Muktasari:

  • Wadau, wagonjwa wa kifafa wamekutana kujadili changamoto ikiwemo unyanyapaa wataka wapewe kipaumbele kama wanavyopewa wenye, Ukimwi, kifua kikuu, saratani.

Dar es Salaam. Unyanyapaa, dawa, huduma, ajira na kipaumbele ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanaougua ugonjwa wa kifafa.

Pia, ukatili, kukosa msaada, ajira, masomo, kuvunjika kwa ndoa imeendelea kuwa mwiba kwao kutokana na hali waliyonayo ya kuanguka bila kutarajia.

Hayo yote wameyaeleza leo Alhamisi Agosti 8, 2024 kwenye kikao kilichoandaliwa na Taasisi ya Wazazi wa Watoto Wenye Kifafa (Uwakita) pamoja na Taasisi ya Waandishi wa Habari za Afya ya Akili Tanzania (TAMHJO) kilichofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam Kitengo cha Afya ya Akili.

Kikao hicho kilichohusisha wadau wa kifafa ni mwendelezo wa kampeni ya kuhamasisha uelewa juu ya ugonjwa huo yenye dhumuni la kutokomeza unyanyapaa, kuelimisha na kupata tiba sahihi.

Akizungumza mmoja ya mwathiriwa wa kifafa, Isrey Ayoub amesema anaishi na hali hiyo kwa miaka sita sasa tangu ianze akiwa kidato cha nne.

"Madhara tunayopata ni mengi ikiwemo, kukosa msaada kwa watu wa karibu kuitwa majina ya ajabu kama tahira, zezeta, mwezi mchanga ambayo yanaumiza.

"Mapendekezo yangu kwa wadau, Serikali na mashirika watupe kipaumbele katika ugonjwa huu kama inavyofanywa kwenye magonjwa mengine kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani," amesema.

Amesema Serikali ianzishe kliniki ya watu wenye kifafa katika ngazi zote za afya kuanzia chini huku akiamini Serikali inaweza na ikianzishwa basi wasichanganywe na watu wa magonjwa ya afya ya akili.

"Aidha, utaratibu mzuri na nafuu wa upatikanaji wa dawa pia, ziingizwe katika mfumo wa bima ili wagonjwa tuweze kupata," amesema Isrey.

Amesema suala la elimu itolewe kwa jamii kusuhiana na hali hiyo ikiwemo namna ya kumsaidia kupitia huduma ya kwanza. Amesema kifafa kinatibika ila sio kwenda kwa waganga bali hospitali.

"Asilimia kubwa ya watu wa kifafa wanahitaji madaktari wa kisaikolojia ili wawabadilishe mitazamo yao ya kutojiamini kutokana na hali waliyonayo," amesema.

Sambamba na hilo, amesema zitolewe fursa sehemu mbalimbali kutokana na ujuzi walionao watu hao kwasababu hawawezi kuwa madereva au mama lishe basi Serikali iwaulize kitu gani wanaweza wawe huru wapewe fursa zingine.

"Natoa wito kwa wenzangu wanaougua kifafa tunapaswa kukubaliana na hali yetu tujiamini," ameongeza.

Fatuma Salum amesema unyanyasaji ni jambo linalomuumiza sana kiasi cha kumfanya aone aibu na kukata tamaa hata katika elimu yake.

Anasema alishapitia changamoto ya unyanyapaa shuleni hata wakati anapata shahada yake ni kutokana na ushauri na msaada alioupata kutoka kwa ndugu zake.

"Wanasema tunaumwa hadi wanafanya tujione waajabu, nitoe rai kwa jamii wasiwe hivi," amesema Fatuma.

Changamoto nyingine ya kimatibabu iliyozungumziwa katika kikao hicho na Daktari wa Afya ya Akili, Jovina Hamis kutoka Hospitali ya Mwananyamala amesema:

"Mgonjwa akitibiwa magonjwa mengine anaambiwa arudi baada ya muda fulani lakini kwa wanaougua kifafa hali ni tofauti hivyo suala hili linapaswa kuangaliwa upya," amebainisha.

Aisia Matowo, mstaafu wa Muhimbili kitengo cha Magonjwa ya akili amesema dhima ya kukutana ni kuelimisha umma kwamba kifafa kinatibika.

"Ni kwamba hapa Tanzania kuna baadhi ya makabila yanaamini kifafa ni kurogwa, mashetani, umizimu, pepo, ndomana tumekutana ili tutoe elimu kuhusu ugonjwa huu ili watu waende hospitali," amesema Matowo.

Aidha, Matowo ameongeza unyanyapaa haufai na jamii iwachukulie watu wenye hali hiyo kama wagonjwa wa kawaida.

Mwanasaikolojia tiba, Alex Ndagabwene, amesema kwa hali aliyoiona kuna watu wanachangamoto ya kifafa hivyo elimu inapaswa kutolewa ikiwemo kuanzia shuleni.

Aidha, Luciana Haule, Daktari kutoka Mkuranga amesema ugonjwa wa kifafa unawagonjwa wengi ambao wanaanzia kwa waganga wa kienyeji ingawa kwa sasa wameanza kupata uelewa wa kwenda hospitali.


Mwarobaini

Mwenyekiti wa Uwakita, Dk Saidi Kuganda amesema watafanya vikao na watu wa wizarani kuwaeleza changamoto hizo ili kuzitafutia mwarobaini.

"Tumeshafanya mazungumzo pia na wadau na watunga sera ili kubadilisha na kuzirekebisha sera hizo ili iwasaidie wanaoishi na hali hiyo," amesema Dk Kuganda.

Ijapokuwa suala la sera si la siku moja amesema wanaamini ndiyo mwarobaini. Amesema changamoto ndogondogo za kuhamasishana na elimu, kubadilisha mitazamo, wanazifanya wao wenyewe.

Daktari wa Afya ya Akili na Mratibu wa Afya ya Akili Kinondoni, Mwendo Peter amesema changamoto wanazozipata wagonjwa zinapaswa kutatulia ili kuboresha hali ya huduma kwa watu hao.

Elimu inapaswa itolewe kwa wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii (CHW) ili kulitekekeza hilo kwanza, wakishapata elimu ya kutosha kuhusu kifafa basi watawasaidia wanajamii wa kawaida.

"Pia tuwape elimu ya kutosha viongozi wetu wa Serikali za mitaa wanapokuwa na ufahamu mzuri na wao wataitoa kwa wananchi. Pia elimu kwa watoa huduma wapate mafundisho ya ziada," amesema.

Amesema ni vizuri Serikali, watoa huduma na jamii zikatambua kuwa elimu kutoka ngazi ya zahanati ni nzuri na inawapa wananchi uelewa wa mapema kuliko kusubiri kwenda ngazi ya juu japokuwa changamoto wataalamu hao wako wachache.

"Sera zetu pia tungeangalia kwa mfano sasahivi inasema huduma za mgonjwa apewe dawa bure lakini kwa wakati mwingine inakuwa ngumu kwani Serikali inapata mzigo mkubwa kuzinunua dawa hizo na wakati mwingine zinapelea," amesema Dk Peter.

Aidha, katika kikao hicho wameazimia wahudumu wanaotoa huduma kwa wagonjwa waelimishwe, kuwapa fursa wanaougua ugonjwa huo wajitokeze, jina la kliniki inayowashughulikia watu hao liangaliwe upya.


Nyongeza na Victoria Michael