Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaodaiwa kuiba Sh5.7 bilioni, bado wanajadiliana na DPP

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo kuiibia benki Sh5.7bilioni, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne.

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025, makao makuu ya benki ya Equity Tanzania Limited yaliyopo Ilala.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa tisa wanaokabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni, umeiambia Mahakama kuwa mchakato wa majadiliano dhidi ya washtakiwa hao, bado unaendelea.

Januari 22, 2026 washtakiwa hao walimuandika barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), wakiomba kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo na mpaka sasa bado wanaendelea na majadiliano.

Wakili wa Serikali, Titus Aron ametoa taarifa hiyo leo Jumatano, Mei 13, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Jasmine Elphas ambaye alikuwa ofisa wa benki ya Equity makao makuu na mfanyabiashara, Fredrick Elphas Ogenga.

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo kuiibia benki Sh5.7bilioni, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne.

Wengine ni  Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, wote ni wafanyabiashara.

Kwa pamoja wanaokabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.

Wakili Aron ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.

"Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na ipo katika mchakato wa majadiliano na washtakiwa kwa ajili ya kuimaliza kesi hii," amedai wakili Aron na kuongeza;

"Na pia, mshtakiwa wa pili katika kesi hii( Fredrick) bado hajakamilisha masharti tuliyokubaliana ya kuimaliza kesi hii, hivyo kwa sababu hiyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili mshtakiwa huyu kukamilisha masharti hayo, lakini pia kuangalia iwapo washtakiwa wengine nao kama wameshakamilisha masharti ya majadiliano," amesema Aron.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, wakili wa utetezi Benedicta Beda, Steven Mosha na Faraja Ramadhani, walikubaliana na ombi hilo.

Aprili 29, 2026 wakili wa Frederick, Meshack Dede aliipa taarifa mahakama hiyo kuwa tayari ameshafanya malipo ya zaidi ya asilimia 50 kwa mshtakiwa wa pili (Fredrick), hivyo aliomba tarehe fupi kwa ajili ya kukamilisha.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 26, 2026 na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana.

Katika kesi ya msingi, kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka la uhujumu uchumi namba 18447 la mwaka 2025.

Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Agosti 30, 2024 hadi Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya jijini Dar es Salaam,  waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh5.7 bilioni mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.

Katika tarehe hizo washtakiwa Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh3.6 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika akaunti ya clearing and settlement mali ya benki ya Equity.

Washtakiwa wengine wanadaiwa katika tarehe hizo, makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, wanadaiwa kuiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.

Pia ilidaiwa, kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025 makao makuu ya benki hiyo, waliiba Sh26 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwemo kuiibia benki Sh5.7bilioni, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne.

Vilevile, kati ya Januari Mosi hadi Aprili 24, 2025 katika benki hiyo, Maina aliiba Sh101 milioni  mali ya benki hiyo.

Ilidaiwa, kati ya Januari 22 hadi Aprili 24, 2025 katika ofisi hizo za benki hiyo  Mohamed, aliiba Sh57 milioni, huku Fata akidaiwa kuiba Sh758 milioni, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2 ,2024 hadi Mei 25, 2025

Mahakama ilieleza kuwa, kati ya Januari 9, hadi Mei 25, 2025, makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, Mrisho aliiba Sh211 milioni, mali ya benki hiyo.

Vilevile ilidaiwa kati ya Januari tisa hadi Mei 28, 2025 makao makuu ya benki hiyo, Neema aliiba Sh32 milioni mali ya benki hiyo.

Mashtaka mengine walidaiwa kuiba Sh108 milioni, mali ya benki hiyo.

Washtakiwa wote, pia wanakabiliwa na mashtaka 10 ya utakatishaji wa fedha walizodaiwa kuiba.