Kortini wakidaiwa kujipatia Sh215 milioni za mafuta ya alizeti
Washtakiwa Desire Hercules na Christian Mbeki, wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa Sola Thierry kwa madai kuwa watasafirisha mafuta ya alizeti kwenda Ufaransa, jambo ambalo walijua kuwa ni uongo.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wawili, Desire Hercules (35), Christian Mbeki (38) maarufu kama Notice Kasaboula, pamoja na kampuni ya Malter Group, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka tisa likiwemo la kujipatia Sh215 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa Sola Thierry kwa madai kuwa watasafirisha mafuta ya alizeti kwenda Ufaransa, jambo ambalo walijua kuwa ni uongo.
Washtakiwa hao ambao wote ni wakazi wa Mbezi Beach, wamefikishwa mahakamani hapo leo Mei 12, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 10131 ya mwaka 2026 na Wakili wa Serikali Titus Aron.
Wakili Aron amewasomea mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Vilevile, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana, hivyo wataendelea kubaki rumande.
Kati ya mashtaka tisa yanayowakabili, matatu ni ya kughushi nyaraka, matatu ni ya kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa, moja ni la kutakatisha fedha, jingine ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na lingine ni la kuongoza genge la uhalifu.
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili Aron alidai katika shtaka la kwanza kuwa washtakiwa wote watatu wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu kwa kutakatisha fedha, shtaka ambalo wanadaiwa kulitenda kati ya Machi 2024 na Juni 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Shtaka la pili ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo mshtakiwa Hercules na Mbeki wanadaiwa kuwa katika tarehe hizo ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walijipatia Dola za Kimarekani 83,625 ambazo ni sawa na Sh215.75 milioni kutoka kwa Sola Thierry kwa madai kuwa watasafirisha mafuta ya alizeti kwenda nchini Ufaransa, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shtaka la tatu ni kughushi nyaraka, ambapo mshtakiwa Hercules na Mbeki wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walighushi nyaraka ya Juni 30, 2024 wakionyesha ni hati halisi na halali iliyotolewa na Chemba ya Biashara Tanzania, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Pia, wanadaiwa kuwasilisha nyaraka hiyo ya Juni 30, 2024 kwa Sola Thierry wakionyesha kuwa ni halali na imetolewa na Chemba ya Biashara Tanzania, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Katika shtaka la tano, Hercules na Mbeki wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho walighushi nyaraka ya Aprili 27, 2024 wakionyesha ni hati halisi na halali iliyotolewa na Chemba ya Biashara Tanzania, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Pia, nyaraka hiyo ya Aprili 27, 2024 waliiwasilisha kwa Thierry wakionyesha kuwa ni halali na imetolewa na Chemba ya Biashara Tanzania, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa katika shtaka la saba, siku na maeneo hayo hayo Hercules na Mbeki walighushi nyaraka ya mwaka 2024 wakionyesha ni hati halisi na halali iliyotolewa na kampuni ya Koln Shipping Line, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Pia, waliiwasilisha nyaraka hiyo kwa Thierry wakionyesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Koln Shipping Line, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shtaka la tisa ni la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote watatu, ambapo katika kipindi hicho ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ovu walijipatia dola za Kimarekani 83,625 ambazo ni sawa na Sh215.75 milioni wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 21, 2026 kwa ajili ya uamuzi baada ya Wakili wa washtakiwa hao, Nehemia Nkoko, kuweka pingamizi dhidi ya Jamhuri kuhusiana na washtakiwa hao kufunguliwa kesi hiyo katika mahakama hiyo.