Wananchi Songea walia makali bei ya sukari

Muktasari:
Bei ya chai kwenye migahawa ya kawaida imepanda kutoka Sh200 hadi Sh500 kwa kikombe kidogo cha chai ya rangi na Sh1,000 kutoka Sh500 ya kikombe cha chai ya maziwa, jambo ambalo si la kawaida kwa wananchi wa mkoani Ruvuma.
Songea. Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamelalamikia kuadimika kwa sukari wakisema bei imepanda kutoka Sh3,800 hadi Sh7,000 kwa kilo, hali inayoongeza ugumu wa maisha.
Malalamiko hayo yamekuja wakati tayari Serikali ilishatoa bei elekezi ya bidhaa hiyo kutoka Sh2,900 hadi Sh3,200 kwa ambayo itadumu kwa miezi sita.
Jana Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa John Bengesi alisema tayari shehena ya sukari imeshawasili na meli bandari ya Dar es Salaam tangu Januari 29 mwaka huu, taratibu za forodha zinaendelea kushusha mzigo huo na kuupeleka sokoni.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 2, 2024 mmoja wa wafanyabiashara wa sukari wa Manispaa ya Songea amesema sukari imeadimika ndio maana bei imepanda.
"Sukari imepanda sana bei, lakini pia imeadimika na hata sisi tumekosa, ila tutaendelea kuwasiliana na wasambazaji," amesema.
Naye Agnetha Focus amesema kutokana na kuadimika kwa sukari bei ya chai imepanda kwenye migahawa ambapo ya maziwa inauzwa Sh1,000 badala ya Sh500 na ya rangi inauzwa Sh500 kutoka Sh200, jambo alilosema sio la kawaida kwao.
Kwa upande wake, Ofisa Biashara wa mkoa huo, Martin Kabaro amesema kuadimika kwa bidhaa hiyo sio suala la Ruvuma pekee, bali ni la nchi nzima, hivyo wameshawasiliana na wasambazaji ili kutatua changamoto hiyo.
"Ni marufuku wasambazaji kuficha sukari na kuuza kwa bei kubwa, kwani Serikali imeshatoa bei elekezi ambapo jumla inauzwa kwa Sh2,900 na Sh3,200 kwa bei ya rejareja.
Amesema Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha sukari inapatikana na kupunguza makali kwa wananchi. “Pamoja na bidhaa hiyo kuadimika wasambaaji hawapaswi kupandisha bei kiholela.”