Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi Kalambo wamtaka DC Lijualikali mbele ya Dk Mwigulu

Muktasari:

  • Wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wananchi hao walipaza sauti mbele ya waziri mkuu wakitaka Lijualikali abaki kwenye wilaya hiyo kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa mkuu wa wilaya, Dk Lazaro Komba ambaye amekuwa mbunge wa Peramiho, Mkoa wa Ruvuma.

Dar es Salaam. Wananchi wa Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa wameonyesha wazi imani yao kwa Mkuu wa Wilaya (DC) anayekaimu, Peter Lijualikali, wakitaka aendelee kubaki katika nafasi hiyo baada ya kuonekana kushughulikia changamoto za wananchi ndani ya muda mfupi tangu aanze kuiongoza wilaya hiyo.

Sauti hiyo ya wananchi ilisikika wazi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumanne, Machi 10, 2026 wilayani humo katika ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ambapo wananchi walipaza sauti wakimtaka Lijualikali aendelee kuhudumu Kalambo kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Lazaro Komba, ambaye sasa ni Mbunge wa Peramiho.

“Mnamtaka huyu, mnasema huyu, sasa huyu akibaki huku halafu kule kwa watu wa Nkasi itakuwaje, haya nimewasikia, nitafikisha salamu kwa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Dk Mwigulu kauli iliyoibua shangwe kwenye mkutano huo.

Hili lilikuja kufuatia Lijualikali ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Kilombero kupitia Chadema (2015-2020) licha ya muda mfupi aliokaimu nafasi hiyo kuonekana kufanyia kazi migogoro kadha wa kadha ikiwemo ya ardhi.

Katika mkutano huo, Dk Mwigulu alimuelekeza Lijualikali kufanyia kazi malalamiko mapya yaliyowasilishwa na mjane Digna Salizandi aliyedai kunyang’anywa mashamba yake na ndugu wa marehemu mume wake.

Digna ambaye ni mjane mwenye watoto sita amesema, baada ya kifo cha mume wake alipokwenda kwenye mashamba yao alikuta wifi na shemeji yake wanalima.

Akitoa maelekezo kuhusu hilo Dk Mwigulu amesema, “Mkuu wa wilaya nenda kalifanyie kazi na hili, kama kweli shamba ni la marehemu na ameacha mke na mtoto, hayo mambo ya mawifi na mashemeji kuchukua hiyo mali ni mambo ya kishamba na kizamani.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Kasanga, Sumbawanga leo Machi 10, 2026 mara baada ya kukagua miundombinu na utendaji kazi wa Bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

“Hayo mashamba ni ya mke na watoto wa marehemu, nyie mlio hai katafuteni mashamba yenu, hii wala haiitaji kusumbua mahakama. Mkuu wa wilaya wakileta ubishi tumia vyombo uwashikishe adabu.

“Huku ni kuonea watu bila sababu na Serikali ipo kwa ajili ya kuwalinda wanyonge wasionewe nikupongeze kwa kuwa tayari umeshaanza kuyafanyia kazi mengine licha ya kuwepo hapa kwa muda mfupi,” amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Lijualikali amesema amebaini uwepo wa migogoro mingi ya ardhi ambayo inatengenezwa na watendaji na watumishi wa Serikali.

“Mara nyingi ardhi ya wananchi inachukuliwa kiubabe, wakidai wanaambiwa ardhi ni mali ya Rais tukitaka tunaichukua kama Serikali na tunajenga. Hali hiyo imeacha migogoro mingi.

“Nimetoa maelekezo kwenye wilaya hii nisisikie popote kauli ya kwamba ardhi hii ni mali ya Rais kwamba tunachukua tunajenga. Nafikiri ifike pahala wanaofanya hivi waelewe kwamba wanamgombanisha Rais na wananchi, Serikali na chama kwa kupora mali yao,” amesema Lijualikali.