Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanakijiji wakumbuka waliyopitia kwa kukosa kituo cha afya

Muktasari:

  • Wakazi wa Kijiji cha Themi ya Simba walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuata huduma kata ya jirani

Arusha. Wakazi wa Kijiji cha Themi ya Simba kilichopo Kata ya Bwawani, Halmashauri ya Arusha, wameeleza masaibu waliyoyapitia walipokuwa wakikosa kituo cha afya kwa zaidi ya miaka 60.

Wamesema walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuata huduma kata ya jirani na usiku hutumia usafiri wa matela ya ng'ombe, baiskeli na punda.

 Mmoja ya wakazi hao, Salome Sarawati amesema alihatarisha maisha yake baada ya kujifungua njiani wakati akiwa safarini kuelekea kituo cha jirani cha Nduruma.

"Nakumbuka ilikuwa mwaka 2017 nilipata uchungu saa tano usiku, nikachukuliwa na baiskeli tulipokuwa njiani hali ikawa mbaya kuna bibi tulikuwa naye ikabidi anisaidie kujifungua pembeni mwa barabara tena usiku.

"Tukarudi nyumbani nikashindwa hata kwenda hospitali baada ya kujifungua, jambo la kushukuru sikuwa na tatizo lolote ila wenzangu wenye matatizo baada ya kujifungulia majumbani wengine wamekufa," amesimulia.

Amesema wajawazito wamekuwa wakijifungulia kwa wakunga wa jadi, pia wamekuwa wakiamshana usiku miaka yote kusaidiana kutokana na eneo lao kukosa huduma hiyo.

“Serikali ituletee sasa vifaa na watumishi ili huduma zianze kutolewa. Kwa sababu haitakuwa na maana kama majengo mazuri ila huduma zikachelewa kuanza,"amesema.

Madina Mustapha amesema si wajawazito hata wagonjwa ambao wamekuwa wakihitaji matibabu, wamepata shida kwa kukosa kituo cha afya, hivyo kutumia gharama kubwa kuzifuata maeneo mengine.

Hussein Said, amesema wamekuwa wakitumia kituo cha afya cha kata ya jirani ya Nduruma.

"Tumekuwa tukitembea kwenda Kata ya Nduruma na hadi mfike huko lazima mpitie magumu njiani," amesema.

Msingi wa wakazi hao kusimulia masaibu waliyopitia unakuja baada ya Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kujenga kituo cha afya kijijini hapo kitakachowahudumia watu zaidi ya 20,000.

Simulizi hizo walizitoa jana Jumatatu, Julai 15, 2024 wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha akiwa na ujumbe wa Tasaf ukiongozwa na mkurugezi mtendaji wake, Shedrack Mziray kutembelea Kituo cha Afya cha Themi ya Simba.

Kituo hicho kinachotarajia kuhudumia wakazi wa eneo hilo pamoja na wa maeneo jirani ikiwemo Wilaya ya Simanjiro kinatarajia kuanza kutoa huduma Septemba mosi, 2024.

Akitoa maelezo ya kituo hicho, Mziray amesema Tasaf imekuwa ikifanya miradi ya elimu, afya na miundombinu kuwawezesha Watanzania.

"Wananchi wa hapa walitambua wana changamoto ya huduma ya afya kwa sababu wamekuwa wakitembea umbali mrefu zaidi kufuata huduma, hivyo na Tasaf tukaona tuwaunge mkono katika mradi huu.

"Mradi huu umegharimu zaidi ya Sh600 milioni na wananchi pia wamechangia nguvu yao kama ilivyo miradi yetu wanachangia asilimia 10. Tuna hakika mradi huu utawanufaisha wananchi wote wa hapa," amesema.

Amesema madhira ambayo wananchi waliyapitia yanakwenda kuwa historia na hilo ndilo lengo la Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha inatambua matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amesema wakazi wa Kata ya Bwawani wamekuwa wakienda kituo kilichopo kata ya Nduruma na maeneo mengine kufuata huduma.

Amesema kituo hicho cha afya kipya chenye majengo manne, kitatanua wigo wa huduma za afya katika halmashauri hiyo.

"Kuna wilaya ya jirani na Simanjiro pamoja na vijiji vinne vya Bwawani, Themi ya Simba Mungushi na Kigongoni katika kata hii ambavyo vyote vitategemea hapa na kuhusu mochwari tumeweka mpango wa kuijenga," amesema Msumi.

Diwani wa Bwawani, Justine Siray amesema kutoka kata hiyo hadi mjini ni kilomita 55, kutafuta huduma ya afya maeneo mengine kumewafanya wakazi hao kutaabika kwa muda mrefu.

"Naishukuru Serikali, Tasaf yenyewe kwa kutujengea kituo hiki, tunachoomba tupate kichomea taka, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na wodi ya kinababa na kinamama," amesema diwani huyo.

Kuhusu hilo, Msumi amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2024/25 watahakikisha wanajenga kichomea taka, kuweka uzio ili kutoruhusu mifugo kuingia, ulinzi pamoja na jengo la mochwari.