Wanafunzi, wazazi wamwangukia Rais Samia matokeo yaliyofutwa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Wanafunzi 140 wa shule ya sekondari Thaqaafa ya jijini Mwanza waliofutiwa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala lao ili wapate fursa ya kurudia mitihani hiyo.

Mwanza. Wanafunzi 140 wa shule ya sekondari Thaqaafa ya jijini Mwanza waliofutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka jana wamemwomna Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati kwa kuziagiza mamlaka husika kuwapa fursa ya kurudia kufanya mitihani ya kidato cha nne.

Wakazungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatano Machi 22, 2023, wnafunzi hao ambao ni miongoni a wanafunzi 337 waliofutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka jana wamesema fursa ya kufanya mitihani hiyo itawawezesha kutimiza ndoto zao kielimu na kimaisha. Jumla ya wanafunzi 560, 335 walifanya mitihani hiyo mwaka jana.

Ombi la wanafunzi hao linakuja wiki kadhaa tangu Waziri wa Elimu, Profesa Adolph Mkenda akutane na wazazi na walezi wao jijini Mwanza Februari 19, mwaka huu na kuahidi kuwa Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa kuwapa fursa ya kurudia mitihani hiyo.

Peter Andrew, mmoja wa waathirika wa tukio la kufutiwa matokeo mwenye ndoto ya kuwa daktari wa binadamu amesema matokeo yake kufutwa imefuta ndoto yake kwa sababu hadi sasa yeye na wenzake hawafahamu hatima yao.

“Kwa upande wetu sisi wanafunzi tulisoma kwa bidii na kufanya mitihani ipasavyo na kwa kwa uaminifu,” anasema Peter

Anasema hata wazazi na walezi wao walijitolea kwa hali na mali kulipia gharama zote katika shule binafsi kwa lengo la kuwaandalia misingi ya maisha bora ya baadaye, lakini lengo hilo limetiwa doa baada ya matokeo yao kufutwa.

“Tunamwomba Rais Samia atusaidie,” anasema Peter akionyesha uso wa huzuni na kukata tamaa

Mwanafunzi mwingine, Joba Sai anasema kufutiwa matokeo kunawafanya wawe wamepoteza bure miaka minne waliyosoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne pamoja na milioni ya fedha zilizolipwa na wazazi na walezi wao.

Mmoja wa wazazi, Simon Tembe amesema kufuta matokeo kumekatisha ndoto za mmoja wa watoto wanaoishi mazingira magumu amabye yeye alijitolea kumlipia gharama zote za masomo anayetamani kufikia kiwango cha juu cha elimu ili baadaye arejee kuwasaidia wenzake wanaoendelea kuishi mazingira magumu mitaani.

Pamoja na kumwomba Waziri Profesa Mkenda kutoa jibu la maamuzi ya mwisho wa Serikali, mzazi huyo amemwomba Rais Samia kuingilia kati suala hilo kunusuru ndoto za wanafunzi hao zinazoelekea kupotea.

“Wazazi tuko tayari hata kuchangia gharama kuwezesha watoto wetu kurudia mitihani,” anasema mzazi mwingine, Upendo Alfred.