Wanafunzi washindwa kwenda shuleni kwa kukosa maji kufulia sare

Muktasari:
- Wakazi wa Kijiji cha Ruyaya wameiomba Serikali iwatengenezee jenereta lao lililoharibika zaidi ya mwaka mmoja ili liwasaidie kuondokana na changamoto ya maji umeme unapokatika.
Kilwa. Wakazi wa Kijiji cha Ruyaya wilayani Kilwa mkoani Lindi wanaiomba Serikali iwatengenezee jenereta lililoharibika zaidi ya mwaka mmoja wanaamini likitengenezwa litasaidia kuondoa changamoto hiyo kijijini humo.
Wamesema kutokana na hali ya kukatika katika kwa umeme kunakosababisha kukosekana kwa maji kijinini hapo kama jenereta lingekuwapo kusingekuwa na changamoto ya kukosekana kwa huduma hiyo.
"Ni kweli kuna tatizo kubwa la maji tuna siku tatu hatunywi maji kwa sababu ya kukosa umeme na jenereta ni bovu zaidi ya mwaka tuliambiwa tutoe laki moja tuwape Ruwasa, tumewapatia lakini hadi leo kifaa hicho hakijatengenezwa. Tunapowauliza wanatuambia subirieni umeme," amesema Mussa Sielewi. ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Ruyaya.
Shamsa Gulamu amesema hapo awali umeme ukikatika walikuwa wanachota maji kwenye madimbwi lakini kwa sasa yamekauka.
"Tunaamka saa tisa alfajiri kuweka foleni yakusubiria maji unafika hadi saa sita hujapata tunaomba watusaidie jenereta hasa kipindi hichi cha shida ya umeme," amesema Shamsa ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ruyaya.
Naye, Hawa Nahani amesema watoto wake wawili leo wameshindwa kwenda shuleni kwa kukosa maji ya kufulia sare za shule na nyumbani sina hata maji ya kupikia chai.
"Jenereta tangu liharibike ni zaidi ya mwaka, kutokana na ukame, madimbwi yamekauka tunategemea chanzo kimoja tu cha maji ya bomba jenereta lingekuwa zima lingetusaidia kutatua hii changamoto," amesema Ally Hassani.
Pia Fahadi Debe amesea anaiyomba Serikali iwasaidie jenereta kwani watu wanakaa hadi saa sita usiku wakisubiria maji ndoa zinaingia mashakani akina mama wanapigana wakiwa wanasubiria maji, wakati jenereta lipo hakukuwapo na hizi changamoto zilizopo sasa.
Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini wilayani Kilwa, Mhandisi Ramadhani Mabula amesema hana taarifa ya kuharibika jenereta na kupelekwa pesa ofisini kwake ili kutengeneza kifaa hicho.
Ameongeza kwa kusema wananchi hao waende katika ofisini zao na taarifa ya maandishi kuonyesha ni nani wamempatia hiyo fedha.