Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi 80 wakacha mtihani wa kidato cha pili Sengerema

Muktasari:

  • Wanafunzi waliosajiliwa mwaka jana kufanya mtihani wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Butonga wilayani Sengerema walikuwa 184, lakini waliofanya mtihani ni 104, sababu zikitajwa ni utoro, ujauzito na kuolewa

Sengerema. Wanafunzi 80 kati ya 184 wa  Shule ya Sekondari Butonga, Halmashauri ya Sengerema Mkoa wa Mwanza, hawajafanya mtihani wa kidato cha pili mwaka jana kutokana na utoro na kupata ujauzito.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Julai 22, 2024 kwenye mkutano wa Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwenye Kijiji cha Butonga Kata Igulumiki wilayani Sengerema.

Mkuu wa shule hiyo, Elias Luhangija amesema changamoto yao ni utoro kwa wanafunzi, huku akiwataka wazazi na walezi kuwahimiza watoto wao kwenda shule.

Luhangija  amesema shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 381 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na walimu 24.

Hata hivyo, Tabasamu amemwagiza Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igulumiki, Renatus Mkama kuwasaka wazazi na walezi wa watoto ambao hawapo shuleni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

"Sikubaliani na utoro, wazazi  wasakwe na kuchukuliwa hatua,” amesema Tabasamu.

Kwa upande wake, Mkama amekiri kupokea majina ya wanafunzi ambao hawakufanya mtihani wa kidato cha pili na kuanza msako wa nyumba kwa nyumba bila mafaniko.

Kata ya Igulumuki ina wakazi 13,705, kaya 1,485, vitongoji 21 na vijiji vitatu vya Butonga, Igulumuki na Ijinga wanaojihusisha na kilimo na ufugaji.

Hamis Maige, Mwenyekiti wa Jumaiya ya Wazazi CCM Kata ya Igulumiki, amesema mwamko mdogo wa elimu kwa wakazi wa kata hiyo ndiyo sababu ya wanafunzi hao kushindwa kuendelea na masomo.

Maige amesema walikuwa wakihamisha wazazi kuwapeleka watoto shule, lakini walikumbana na masuala yanayokatisha tamaa wakidai wasomi wapo wengi na hawana ajira, hivyo ni bora walime na si kusoma.

Mkurungezi wa Halmashauri ya Sengerema, Binuru Shekidele amesema kabla ya wanafunzi hawajafanya mitihani walipata taarifa ya utoro  ikiwamo Shule ya Sekondari Butonga.

Amesema walifika Kijiji cha Butonga kuzungumuza na wananchi juu ya kupeleka watoto shule kutokana na kutokuwa na mwamko wa elimu.

"Tutaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kupeleka watoto shule, elimu ndiyo ufunguo wa maisha kwa binadamu katika ulimwengu huu,” amesema Shekidele.