Wanafunzi 1,050 kunufaika na ufadhili wa masomo wa Samia Scholarship
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo Jumatatu Julai 26, 2026. Pich na Elidaima Mangela
Muktasari:
- Ufadhili huo ni wa hiari hivyo wanafunzi hao watatakiwa kujaza fomu za kuthibitisha kama wamekubali ikiwemo na hao 50 ambao watatakiwa kuweka kambi kwa mafunzo ya ziada katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha jijini Arusha.
Dodoma. Wanafunzi 1,050 wamechomoza katika alama zilizowawezesha kupata ufadhili wa masomo kwa shahada ya kwanza, maarufu kama Samia Scholarship ambapo 50 kati yao watakwenda kusoma nje ya nchi na wengine 1,000 watasoma vyuo vya ndani.
Hata hivyo, ufadhili huo ni wa hiari, hivyo wanafunzi hao watatakiwa kujaza fomu za kuthibitisha kama wamekubali ikiwemo na hao 50 ambao watatakiwa kuweka kambi kwa mafunzo ya ziada katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha jijini Arusha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewaambia waandishi wa habari leo Jumatatu Julai 27, 2026 kuwa ufadhili huo umewalenga wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi katika mitihani ya kidato cha sita na ambao wapo tayari kusoma masomo yenye kipaumbele.
“Hawa 1,000 ambao wataona majina yao leo kwenye tovuti, watatakiwa kujaza fomu za kuthibitisha vyuo na watalipiwa asilimia 100, na wale 50 nao majina tunaweka kwenye tovuti leo, lakini utaratibu wao itakuwa ni kwanza wathibitishe na kukubali kwamba watakaa miezi 10 pale Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST),” amesema Profesa Mkenda.
Ametaja sababu ya wanafunzi 50 kuchelewa kwa miezi 10 ni utofauti wa kuanza kwa mihula ya masomo katika vyuo wanavyopelekwa, hivyo muhimu wakaanza na mafunzo maalumu ikiwemo kuwajengea uwezo wa kizalendo.
“Tunawapeleka ili kuwaandaa, kuwa mabalozi wazuri wa mila na desturi za Kitanzania, na tunatumia muda huu kutokana na baadhi ya vyuo vilivyopo nje ya nchi tunavyowapeleka kuchelewa kuanza muhula wa masomo,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema katika kipindi hicho, wanafunzi hao hufundishwa masuala ya uzalendo, maadili na namna ya kulinda na kuendeleza utamaduni wa Taifa na kuongeza ujuzi katika Tehama kwani baadhi ya shule walizotoka hazina kompyuta, hivyo lazima waanze kujifunza hapo ili kuhakikisha wanapokwenda kusoma nje ya nchi wanakuwa mabalozi wazuri wa Tanzania.
Kwa upande mwingine, Waziri amefungua milango kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi ambao wanahisi walikuwa na ufaulu wa juu lakini wameachwa, wanaweza kufuatilia ukweli huo na wizara itawapa ushirikiano kwa Baraza la Mitihani ili kujiridhisha kwani wasingetamani kuwepo na ubabaishaji wa waliochukuliwa.
Amezungumzia uwiano wa kuchukuliwa kwa wanafunzi ambapo asilimia 58 wamechukuliwa kutoka shule za sekondari za umma na asilimia 42 wametoka shule za sekondari za binafsi.
Kuhusu watakaoshindwa kuingia kwenye makubaliano ya ufadhili huo, amesema Serikali kwa haraka itawachukua wengine ambao wamekuwa na ufaulu lakini kwa sababu ya kigezo cha idadi walikuwa wameachwa.