Wamiliki wa ardhi 636 wakutwa na deni

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya ardhi kutoka Taasisi za Dini, Makampuni na Watu binafsi katika ukumbi wa Shirika la Nyumba jijini Dar es Salaam Machi 05, 2025.
Muktasari:
- Ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya ukusajai wa maduhuli ya Sh 250 bilioni wadau wa ardhi wameeleza changamoto inayokwamisha ulipaji wa madeni ya pango la ardhi na kujikuta wakiwa na malimbikizo makubwa yaliyotokana na riba ya ucheleweshaji wa malipo.
Dar es Salaam. Jumla ya wamiliki wa ardhi 636 wamehakikiwa na kubainika kuwa na deni la pango la ardhi la thamani ya Sh44 bilioni zikiwepo kampuni 18, taasisi za umma na binafsi pamoja na watu binafsi.
Deni hilo ni la msingi pamoja na riba ya malimbikizo ambapo Mkoa wa Dar es Salaam deni lake ni Sh28 bilioni na Pwani ni Sh 16 bilioni.
Wadau wa sekta ya ardhi wakizungumza leo Machi 5, 2025 katika kikao kazi cha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Ardhi jijini Dar es Salaam, wamesema kinachochangia kuwa na malimbikizo ya madeni ni kuwepo kwa mashauri ya migogoro ya ardhi na mfumo wa ulipaji wa kodi sio rafiki.
Mdau wa ardhi kutoka Bagamoyo, Ludovick Shirima amesema ulipaji wa kodi ya pango la ardhi uwe bayana ambao utamfanya mlipaji kulipa kwa urahisi tofauti na wasasa ambao unatoa mwanya wa kuwepo kwa utoaji wa rushwa.
"Ukiangalia sio rahisi kwa mlipa kodi kwa utaratibu uliopo wa kuwasilisha haya maduhuli kwa Serikali, hili eneo Wizara na idara zake wanatakiwa kuweka wazi siku, muda na sehemu ya kulipia hili ni tatizo kubwa kwa sababu uwazi uliopo sio rafiki na unasabbaisha watu kuchelewa kulipa,"amesema Shirima.
Naye, Hellen Masanja, kutoka Bagamoyo amesema kumekuwa na uvamizi wa matapeli kwenye maeneo ya watu na kuanza kuuza hali inayosababisha malimbikizo ya madeni kwa sababu ya kusubiri suluhisho ya changamoto zao kupitia halmashauri.
"Sisi wawekezaji tumejikuta kwenye wakati mgumu na kuwa na madeni ya kujilimbikiza kwa sababu kuna kuwa na kesi ambazo zimesababishwa na matapeli wakati huo hatufanyi uzalishaji wowote tukisubiri mashauri yetu yafanyiwe kazi hadi kumalizika unajikuta umepoteza vitu vingi kwa sababu ya kusimamisha uzalishaji," amesema Hellen.
Kutokana na maelezo ya wadau, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema watahakikisha kuna kuwa na mfumo rahisi wa kuweza kufanya mmiliki wa ardhi kulipa kodi yake kirahisi.
"Niwahakikishea kuna kuwa na mfumo rahisi wa kulipia kodi kama ilivyo kwenye taasisi nyingine za umma ya kuja kwa ujumbe wa maneno (Sms), na namba ya malipo inafanyakazi kwa muda ili kuweza kulipa kodi kwa urahisi.
Vilevile amewataka wale wote wenye mashauri kwenye halmsahuri na mahakama ambayo hayajapatiwa ufumbuzi waandike barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara Ardhi au kwa Waziri kwa ajili ya kuelezea wameshindwa kulipa kwa sababu ya kutopata uhakika wa umiliki wa ardhi hadi mashauri yao yatakapokuwa yamefikia mwisho.
Amesema ili na wao waweze kujua na kusimamisha wadaiwa wa pango la ardhi hadi itakapothibitika uhalali wa umiliki na kuweza kulipa deni lake.
Pia, amechukua ombi la kutolewa kwa riba na kulipeleka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa riba na tozo zilizokuwa kwenye kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa na kulipa deni halisi kama alivyofanya mwaka 2023/24.
Amewataka wadaiwa kulipa deni halisi wakati anaenda kuomba ombi lao hilo kabla ya mwaka wa fedha 2024/25 kumalizika ili kuonyesha ombi lao lilikuwa kikwazo na kuweza kufikia mwisho.
Mbali na hilo, amesema kwa wale ambao wamegawanya maeneo na viwanja kupimwa lakini vipo kwenye hati kubwa moja ni vema kuandika barua mapema kwa kamisha japokuwa haiondoi deni wanalodaiwa.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Lucy Kabyemera amesema lengo kukutani ni kujadili namna bora la utekelezaji wa takwa la kisheria la ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.
Amesema kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 Wizara imepewa jukumu la kukusanya maduhuli ya Serikali ya Sh 250 bilioni, ili kufikia malengo hayo hadi kufikia Februari 28, 2025 wamekusanya Sh 105 bilioni sawa na asilimia 42 ya lengo.
"Kwa kuzingatia tunafikia malengo tuliopangiwa Wizara imeratibu na kupanga utekelezaji wa mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali iweze kufanikiwa kwa ufanisi,"amesema Lucy.
Amesema kukutana na wamiliki wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi ni njia mojawapo ya kuona namna ya kurahisisha mkakati wao na kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa mapato unaotokana na sekta ya ardhi.
Amesema awamu ya kwanza imeanza kwa kuwafuqtalia walipa kodi wakubwa na timu ya wataalamu wameshiriki kwenye shughuli ya ukusanyaji madeni tangu Februari 25 mwaka huu kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Mwanza na Shinyanga mpango uliopo ni kuwafikia wadaiwa nchi nzima.
"Utaratibu wa kuwafikia wadaiwa umejikita katika maeneo mahususi ikiwepo wamiliki kupatiwa ilani ya kuwataka kulipa madeni yao na wadaiwa wakubwa kulipa madeni yao kwa awamu,"amesema.
"Hata hivyo fursa hiyo inatolewa baada ya mmiliki kujaza hati ya makubaliano ya kuwajibika kulipa deni husika na kuchukua hatua kwa wahusika watakaoshindwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ambayo ni Na 4 ya mwaka 1999," amesema.