Walioomba ajira Polisi majina haya hapa

Muktasari:
- Wenye Shahada, Stashahada, na Astashahada Tanzania Bara watasailiwa DPA Kurasini, na wenye elimu ya sekondari kwenye mikoa waliyotaja. Zanzibar usaili utafanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na Pemba. Wote wataletewa vyeti halisi na vitambulisho.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mmoja wa wale walioomba ajira Jeshi la Polisi majina yao yameshatoka na usaili utaanza kufanyika Julai 29 hadi Agosti 11, mwaka huu.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi anapenda kuwatangazia kuwa vijana walioomba ajira ya Jeshi la Polisi kupitia mfumo wa Ajira Tanzania Police Force Recruitment Portal, usaili wao utafanyika kuanzia Julai 29, 2024 hadi Agosti, 2024 nchini kote,” inaeleza taarifa hiyo.
Waombaji wa Tanzania Bara wenye elimu ya Shahada, Stashahada na Astashahada usaili wao utafanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA) kilichopo Barabara ya Kilwa (Kurasini).
Aidha, wenye elimu ya kidato cha nne na sita usaili wao utafanyika kwenye mikoa waliochagua wakati wa kutuma maombi.
Waombaji wa Zanzibar wenye elimu ya Shahada, Stashahada, Astashahada, kidato cha sita na nne usaili utafanyika Zanzibar. Walioko mikoa ya Unguja usaili utafanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na mikoa ya Pemba usaili utafanyika Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba (Chakechake).
Pia, waombaji wametakiwa kila mmoja kufika akiwa na vyeti halisi vya taaluma (academic certificates), cheti cha kuzaliwa, kitambulisho cha Mamlaka ya Utambulisho wa Taifa (Nida) au namba ya utambulisho wa Taifa Nida, nguo na viatu vya michezo.
Jeshi hilo pia limesema atakayefika kwenye usaili baada ya Julai 2024 hatopokewa.