Wakunga, wauguzi waonywa kupokea zawadi kutoka kwa wagonjwa

Mkurugenzi wa mafunzo na maendeleo ya wataalamu wa sekta ya afya kutona wizara ya afya, Dk. Saitore Laizer akizungumza na wasichana waliohitimu kozi ya uuguzi na ukunga kupitia ufadhili wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Camfed. Picha Hamida Shariff, Mwananchi
Muktasari:
- Mkurugenzi wa mafunzo na maendeleo ya wataalamu wa sekta ya afya kutoka Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer amesema rushwa siyo tu fedha ile inayotolewa ama kupokewa kabla ya kutoa huduma, bali hata ile inayotolewa au kupokewa baada ya huduma.
Morogoro. Wauguzi na wakunga nchini wameonywa kupokea fedha au zawadi kutoka kwa wagonjwa au ndugu wa wagonjwa baada ya kuwapa huduma kwani kitendo hicho kinatafsiriwa kuwa ni rushwa na siyo motisha kama ambavyo inafahamika kwa baadhi ya watu.
Onyo hilo limetolewa leo Aprili 11, 2024 na mkurugenzi wa mafunzo na maendeleo ya wataalamu wa sekta ya afya kutoka Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer wakati akifungua jukwaa la wahitimu wa kozi ya uuguzi na ukunga.

Wasichana waliohitimu kozi ya uuguzi na ukunga kupitia ufadhili wa Shirika la Camfed wakimsikiliza Mkurugenzi wa mafunzo na maendeleo ya wataalamu sekta ya afya Dk. Saitore Laizer alipokuwa akizungumza na wauguzi hao kutoka vyuo 20 vya hapa nchini. Picha Hamida Shariff Mwananchi
Wahitimu hao walikuwa wakifadhiriwa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kampeni ya elimu kwa wasichana la Camfed ambapo wauguzi na wakunga 274 walihitimu na wako tayari kufanya kazi hiyo.
“Rushwa sio tu fedha ile inayotolewa au kupokelewa kabla ya kutoa huduma, bali hata ile inayotolewa ama kupokewa baada ya kutoa huduma. Kama mgonjwa ameridhika na huduma uliyompa na anataka kukupa ‘asante’, basi ataweza kutafuta siku nyingine na mahala pengine pa kukupa na siyo maeneo ya kazi.
“Wewe muuguzi ama mkunga, ni wajibu wako kutoa huduma bora kwa magonjwa, epukeni kupokea rushwa,” amesema Dk Laizer.
Amewataka wauguzi na wakunga kuepuka kutoa lugha chafu na zisizokuwa na staha wa wagonjwa balada yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili na miiko ya kazi ili kuepuka malalamiko kutoka wa wagonjwa lakini pia kulinda heshima ya taaluma hiyo ambayo inategemewa katika sekta ya afya.
Kaimu mkurugenzi msaidizi idara ya mafunzo Wizara ya Afya Asnath Mpela amesema sekta ya afya inategemea kada ya uuguzi na ukunga katika kutoa huduma za afya.
“Asilimia 80 ya kuduma za afya kwenda zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya na za rufaa za mikoa zinafanywa na wauguzi na wakunga, hivyo kada hii ni muhimu, nasema hivyo kwa sababu na mimi pia ni muuguzi nalijua hilo," amesema Mpela.
Amewashauri wauguzi na wakunga waliohitimu kozi hiyo kujitolea kwenye zahanati na vituo vya afya vilivyokuwa karibu yao ili waweze kupata ujuzi na umahiri katika kada hiyo badala ya kusubiri ajira.
Akitoa taarifa ya ufadhili wa wahitimu hao ambao ni wasichana waliokuwa wakiishi kwenye mazingira magumu, ofisa na mratibu wa mradi wa ufadhili, Tukaeje Mzeru amesema Camfed imetumia zaidi ya Sh4.2 bilioni kufadhili wanafunzi 298 wa kozi ya uuguzi na ukunga.
Amesema kati ya wahitimu hao, 257 walifanya mitihani yao ya mwaka wa mwisho na kufaulu vizuri huku 16 wakiendelea na masomo ya kurudia baadhi ya moduli kutokana na changamoto mbalimbali.
Mzeru amesema katika ufadhili huo wanaoutoa, wapo wanafunzi 25 ambao hawakufanikiwa kumaliza programu kwa sababu mbalimbali ikiwemo ikiwemo kupata ujauzito, kuahirisha masomo na kubadilisha kada na sababu nyingine za kifamilia.

Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Camfed Nasikiwa Duke akitoa taarifa ya ufadhili wa wasichana 298 waliopata ufadhili kupitia Shirika hilo kusoma kozi ya uuguzi na ukunga. Picha Hamida Shariff Mwananchi
Awali, Mkurugenzi wa Shirika la Camfed, Nasikiwa Duke amesema mwaka 2021 shirika hilo lilipata ufadhili kusaidia wasichana wanaotoka kwenye mazingira hatarishi wanaosoma kozi ya uuguzi na ukunga kwa programu ya miaka mitato.
Duke amesema lengo la ufadhili huo ni kuongeza idadi ya watumishi wa sekta ya afya hasa katika maeneo ya vijijini ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa ujauzito na kujifungua.
“Camfed kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya ilikubali programu ifike kwenye vyuo vya afya 20 ambapo wanafunzi walikuwa wakipewa ufadhili kwa kugharamia ada, malazi, chakula, vifaa vya kujifunza, usafiri na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kujikuta katika masomo yao bila ya usumbufu wa kifedha,” amesema Duke.