Wakulima 2,000 kunufaika na vifaa vya kilimo cha umwagiliaji
Muktasari:
- Kati ya wakulima hao, 368 wanatoka mkoani Mara katika kata 15 zilizopo kwenye halmashauri za Musoma Manispaa, Rorya na Musoma Vijijini.
Musoma. Zaidi ya wakulima wadogo 2,000 katika mikoa saba nchini wanatarajiwa kupatiwa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh3.5 bilioni kwa ajili ya kufanya kilimo cha umwagiliaji katika mikoa hiyo.
Kati ya wakulima hao, 368 wanatoka mkoani Mara katika kata 15 zilizopo kwenye halmashauri za Musoma Manispaa, Rorya na Musoma Vijijini.
Akizungumza mjini Musoma leo Jumanne Novemba 11, 2025 wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo kwa wakulima wa Mkoa wa Mara, mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Nyabaganga Talaba amesema vifaa hivyo vinalenga kuboresha kilimo nchini.
Talaba amesema katika programu hiyo wakulima mkoani Mara wamepatiwa seti 34 ya vifaa yenye thamani ya zaidi ya Sh468.4 milioni ili waweze kuboresha shughuli zao za kilimo hasa za mbogamboga na matunda.
"Walengwa wa programu hii ni wale wa kwenye vikundi ambavyo vinafanya shughuli zao kwenye maeneo rasmi ya kilimo cha umwagiliaji, mfano pembezoni mwa vyanzo vya maji lakini kwa kufuata sheria na taratibu za uhifadhi wa mazingira,” amesema.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amewataka maofisa ugani katika halmashauri husika kuhakikisha wanapima afya ya udongo ili wakulima hao waweze kulima kwa tija.
Kusaya amesema Serikali imedhamiria kuboresha sekta ya kilimo nchini ili kiweze kuleta tija kwa wakulima na jamii kwa ujumla hivyo kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
“Hakuna mkulima aliyeombwa fedha ili apate vifaa hivi sasa sote kwa pamoja tuhakikishe vinakuwa sababu ya kuwa na kilimo endelevu chenye tija ili kuboresha hali ya usalama wa chakula, sambamba na kipato cha mkulima na jamii nzima,” amesema Kusaya.
Amesema kutokana na wakulima wengi nchini kukabiliwa na changamoto nyingi Serikali imeweka mipango mikakati mbalimbali ili kuwa suluhisho la changamoto hizo, ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkulima, Majura Mahinya amesema hivi sasa watakuwa na uwezo wa kumwagilia umbali wa zaidi ya mita 500 kwa wakati mmoja tofauti na awali ambapo vifaa walivyokuwa wakitumia vilikuwa na uwezo wa kumwagilia mita 100 pekee, hivyo kusababisha uzalishaji wa mazao kuwa mdogo.
Mkulima mwingine, Joseph Siaga amesema kupatikana kwa vifaa hivyo kutawapunguzia gharama za uendeshaji hasa pesa walizokuwa wakitumia kuwalipa vibarua kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba yao.