Wakili kesi ya kina Dk Slaa amuomba Rais Samia kuingilia kati

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu ameombwa kuingilia kati kumaliza sakata la kukamatwa kwa Dk Slaa, Mwabukusi na Mdude.
Mbeya. Wakili Philip Mwakilima amesema hatma ya wateja wake Boniphace Mwabukusi na Mdude Nyagali pamoja na Dk Wilbroad Slaa kupelekwa mahakamani, huku akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati kumaliza suala hilo.
Wakati wakili huyo akitoa kauli hiyo, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesema litatoa taarifa baada ya taratibu kukamilika.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Mwabukusi na Mdude waliokamatwa Agosti 12 Mikumi mkoani Morogoro wanashikiliwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi, huku Dk Slaa aliyekamatwa Agosti 13 jijini Dar es Salaam akishikiliwa kwa tuhuma hizo.
Tangu walipoanza kushiukiliwa na kufikishwa mkoani Mbeya watuhumiwa hao hawajafikishwa mahakamani kwa kile kinachoelezwa kuwepo kwa mvutano baina ya mawakili na Jeshi la Polisi walishindwa kupandishwa kizimbani.
Hata hivyo, leo Agosti 17 wakili Mwakilima alionekana viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya akihangaika huku na kule akiufutilia hatma ya wateja wake kujua mustakabali wa kufikishwa mahakamani.
Akizungumza nje ya Mahakama hiyo, Mwakilima amesema baada ya kufanya mazungumzo na Polisi, majibu aliyopewa ameona uhalisia wa suala la wateja wake kufikishwa mahakamani kuwa gumu kwani watekelezaji wanazo mamlaka wanazotumikia.
Amesema kutokana na mazingira aliyobaini ameona mwenye uwezo wa kumaliza tatizo hilo ni Rais Samia pekee, huku akieleza kuwa Jeshi la Polisi na wengine wote wanaolalamikiwa ni kuwaonea tu na kutowatendea haki kwani kuna mambo yako nje ya uwezo wao.
"Nimekwenda kwa RPC Kamanda wa Polisi mkoa), RPO (mwendesha mashitaka wa mkoa), wanasema tuwe wavumilivu, maana yake hawa tunawapa lawama bure hata mahakamani hakutakuwa na chochote tunachoomba, ni Rais pekee anayeweza kumaliza hili," amesema.
Amesema hakukuwa na uharaka wa kupeleka nyaraka ili kuliamuru Jeshi la Polisi na Mkuu wa mashtaka ili wateja wao waletwe mahakamani.
"Tumebaini kuna vitu vipo nje ya uwezo wao tutawalaumu bure wote akiwamo RPC, RPO, Askari na kupoteza muda na ni kutowatendea haki kwani zipo mamlaka wanazozitumikia" amesema Mwakilima.
Wakili huyo ameongeza kuwa kadri muda unavyoenda mmoja ya mteja wake Mwabukusi ni mgonjwa akiwa ana mishono mwilini, lakini Dk Slaa ni mzee na amelitumikia Taifa kwa uzalendo na kwamba kuwalaza kwenye sakafu ni kuwatafutia matatizo zaidi.
Ameongeza kuwa kama kuna washauri wanaompa maneno ya uongo Rais Samia ni kulipotezea sifa Taifa na kumchafua kiongozi huyo mkuu wa nchi kwa kutumia vibaya nafasi zao.
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu sintofahamu hiyo, Kamanda msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Anthony Mkwawa amesema bado wanaendelea na taratibu ambapo mambo yakiwa tayari watalitolea taarifa rasmi.
"Kujua hatma yao ni lini au nini kinaendelea tusubiri, bado taarifa haijawa tayari tutakapokamilisha na mambo yakawa sawa tutatoa taarifa," amesema Mkwawa.