Wahamiaji saba kortini, mmiliki wa ‘shangingi’ bado hajatajwa

Muktasari:

  • Walikamatwa Juni 4, 2024 wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T888 BTY aina ya Toyota Land Cruiser.

Moshi/Dar. Raia saba wa Ethiopia, waliokamatwa Njiapanda wilayani Moshi wakisafirishwa kwa gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T888 BTY linalodaiwa kumilikiwa na mbunge, wamefikishwa kortini wakikabiliwa na mashitaka mawili.

Ingawa hati ya mashitaka haikutaja nani ni mmiliki wa gari hilo, vyanzo kutoka Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vinaeleza nyaraka za umiliki wa gari hilo zinasoma jina linalofanana na la mbunge anayetokana na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo gari hilo lilipokamatwa Juni 4, 2024 mbunge huyo hakuwamo kwenye gari bali lilikuwa likiendeshwa na dereva ambaye alitoroka na kuliacha na hadi sasa hajapatikana.

Mwananchi ilifanya kila jitihada kumtafuta kwa simu mbunge huyo bila mafanikio, kwani siku moja alipopigiwa hakupokea ila akatuma ujumbe atumiwe SMS (ujumbe mfupi) lakini alipotumiwa kuuliziwa juu ya sakata la gari lake, hakujibu.

Mwananchi leo Juni 21, 2024 imemtafuta tena kwa simu mbunge huyo, simu iliita bila majibu na kufifisha jitihada za kufahamu kama wakati linakamatwa bado yeye alikuwa mmiliki au lina umiliki wa mtu mwingine ambaye hajafanya mabadiliko ya miliki.

Mara ya mwisho kuzungumza na Mwananchi Juni 5, 2024 Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga alielezea kukamatwa kwa wahamiaji hao akisema wanaendelea na uchunguzi na hawajaweza kubaini gari hilo ni mali ya nani.

"Mpaka sasa tunaendelea na uchunguzi kufahamu mmiliki wa gari ni nani, kwani dereva alikimbia na kwa mujibu wa sheria za nchi gari hilo likibainika kutumika kusafirisha wahamiaji haramu litakuja kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali," alisema.


Wahamiaji kortni Moshi

Wahamiaji hao walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Moshi Juni 14, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi, Rehema Olambo na kusomewa mashitaka mawili na mwendesha mashitaka, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Issack Mangunu.

Washitakiwa hao ni Tensa Matwis, Abi Arose, Buruk Helobo, Arigudo Aromo, Sisy Abera, Mirhetu Sulore na Sharifan Betiso, ambao walikana mashitaka dhidi yao.

Katika shitaka la kwanza, inadaiwa Juni 4, 2024, eneo la Njiapanda katika Wilaya ya Moshi, washitakiwa wakiwa raia wa Ethiopia, waliingia nchini kinyume cha sheria wakitumia gari lenye namba za usajili T888 aina ya Toyota Land Cruiser.

Kosa hilo ni kinyume cha kifungu namba 45(1)(i) na (2) cha sheria ya Uhamiaji sura ya 54 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2016, kosa ambalo walilikana kortini.

Katika kosa la pili, wakili Mangunu alidai siku hiyohiyo katika eneo hilohilo, washitakiwa walikutwa kinyume cha sheria wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini.

Kosa hilo ambalo pia walilikana linaangukia katika kifungu namba 45(1)(i) na (2) cha sheria hiyo ya Uhamiaji.

Washtakiwa walipelekwa mahabusu katika Gereza Kuu la Karanga mjini Moshi hadi Julai 2, 2024 kesi itakapotajwa tena.

Kutokana na mamlaka zenye dhamana ya uchunguzi Mkoa wa Kilimanjaro kushikwa na kigugumizi cha kueleza nani ni mmiliki wa gari hilo, uchunguzi huru wa Mwananchi kupitia nyaraka za bima na TRA, zinasoma jina linalofanana na la mbunge huyo.

Uchunguzi uliofanywa katika tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya www.parliament.go.tz inaonyesha jina lililopo katika tovuti hiyo linashabihiana na lile linalosomeka katika nyaraka za bima na zile za umiliki.

Lakini chanzo kingine kutoka TRA kitengo cha usajili wa magari jijini Dar es Salaam, kiliieleza Mwananchi kwa nyaraka walizonazo, kwa sasa gari hilo linamilikiwa na mtu mwenye jina ambalo Mwananchi linalo, ila hawafahamu kama ni mbunge.

“Mimi sijui kama ni mbunge maana kwenye mfumo haisemi ana wadhifa gani bali inaeleza mwenye gari yenye namba hiyo ni nani na namba ya simu lakini liliingizwa nchini na kusajiliwa katika mfumo mwaka 2016,” kilieleza chanzo cha habari.

Tangu kukamatwa kwa gari hilo na dereva aliyekuwa akiliendesha kutoroka, umma umekuwa ukitaka kufahamu gari hilo ni la mbunge gani japo umma unafahamu hahusiki na tukio hilo.