Sakata gari la mbunge kunaswa na wahamiaji haramu ngoma bado nzito

Muktasari:

  • Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Zablon Walwa amesema kwa mujibu wa sheria, hawana mamlaka ya kutoa taarifa za mmiliki wa gari hilo kwa mtu mwingine tofauti na mlipakodi au mamlaka zilizoidhinishwa.

Moshi. Sakata la kukamatwa kwa gari Toyota Landcruiser V8 linalodaiwa kuwa ni mali ya mbunge likisafirisha wahamiaji haramu saba wa Ethiopia, limechukua sura mpya baada ya Idara ya Uhamiaji Kilimanjaro kudai hawajaweza kubaini mmiliki wake.

Wakati ikiwa imepita zaidi ya saa 24 bila idara hiyo kumbaini mmiliki wake, mmoja wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alilidokeza gazeti hili kuwa kumbaini mmiliki wa gari ni jambo linalochukua chini ya dakika mbili kupitia mfumo.

Mwananchi imefanya jitihada za kumtafuta mbunge huyo ambaye alikuwepo Kilimanjaro tangu wiki iliyopita kwa shughuli za kifamilia kwa kumpigia simu, lakini hakupokea na kutuma ujumbe wa maandishi kuwa atumiwe meseji na alipotumiwa, hajaujibu licha ya kuonyesha ameshausoma.

Ingawa Idara ya Uhamiaji imesema bado wanaendelea na uchunguzi kumbaini mmiliki wake, uchunguzi wa Mwananchi umebaini majina matatu ya mmiliki wa gari hilo ambayo yanafanana neno kwa neno na majina ya mmoja wa mbunge wa Bunge la Jamhuri.

Mbali na mifumo ya bima kuonyesha jina la mmiliki wa gari hilo, lakini majina hayo matatu yanafanana neno kwa neno na majina ya mbunge katika tovuti ya Bunge na wakati gari hiyo ikikamatwa, mbunge anayetajwa hakuwamo ndani ya gari hilo.

Alipotafutwa Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipa Kodi wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Zablon Walwa ili kufahamu nani ni mmiliki wa gari hilo, amesema kwa mujibu wa sheria, hawana mamlaka ya kutoa taarifa za mlipakodi kwa mtu mwingine tofauti na mlipakodi au mamlaka zilizoidhinishwa.

"Kupata taarifa za umiliki wa gari ya mtu, zile ni taarifa za kikodi ambazo kwa matakwa ya sheria, hatuna mamlaka ya ku share (kubadilishana) na mtu mwingine, tofauti na mlipakodi mwenyewe ama mamlaka ambazo zimeidhinishwa,” amesema.

Walwa akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 5, 2024, amezitaja mamlaka hizo kuwa ni pamoja na Polisi na Mahakama, lakini nazo pia zinaomba kwa maandishi kupewa taarifa hizo.


Kauli ya Uhamiaji

Akizungumza jana, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga ameelezea kukamatwa kwa wahamiaji hao wakiwa kwenye gari hiyo na kusema wanaendelea na uchunguzi na kwamba hawajabaini gari hiyo ni mali ya nani.

"Jana (juzi) Juni 4, 2024, tukiwa kwenye majukumu yetu ya kazi maeneo ya Himo tulikamata raia saba wa Ethiopia waliokuwa wakielekea Afrika Kusini. Tunaendelea na taratibu za uchunguzi na baadaye kuwafikisha mahakamani," amesema Nyakunga na kuongeza;

"Mpaka sasa tunaendelea na uchunguzi kufahamu mmiliki wa gari ni nani, kwani dereva alikimbia na kwa mujibu wa sheria za nchi gari hilo likibainika kutumika kusafirisha wahamiaji haramu litakuja kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali."

Mkuu huyo wa Uhamiaji Kilimanjaro amewataka wananchi kuacha kujihusisha na biashara ya wahamiji haramu kwa kuwa magari yatakayobanika kuwasafirisha na nyumba zitakazokutwa zimewahifadhi zitataifishwa.

"Lakini pia mtu atakayekamatwa akifanya biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu anaweza kufungwa jela miaka 20 au kulipa faini ya Sh 20milioni kama adhabu au vyote kwa pamoja akitiwa hatiani, hivyo tujiepushe na biashara hii."

Nyakunga amewataka viongozi wa vijiji na vitongoji waishio maeneo ya mipakani na mijini kubaini nyumba ambazo haziishi watu kwa kuwa zinatumika kama maficho ya wahamiaji haramu.

"Nitoe wito pia kwa madereva wa magari ya abiria ambao wakati mwingine husafirisha wahamiaji haramu na hata mama lishe ambao wakati mwingine huwapelekea chakula, waache mara moja au kutoa taarifa kwa mamlaka,” amesema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipoulizwa juu ya tukio hilo alijibu kwa kifupi, “Ni kweli tumewakamata wahamiaji haramu, lakini tumewakabidhi uhamiaji. Wasiliana na uhamiaji kwa taarifa zaidi.”


Gari lilivyokamatwa

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, wahamiaji hao walikamatwa Juni 4, 2024 kati ya saa 1:30 na saa 2:30 katika eneo la maegesho ya magari ya hoteli iliyopo Njiapanda, Barabara ya Moshi-Dar es Salaam, ingawa dereva alifanikiwa kutoroka.

Kulingana na vyanzo hivyo, dereva wa gari hilo alifika katika eneo hilo la maegesho na kuliegesha hapo akiwaaga wateja wake kuna anakwenda kununua vocha kwa ajili ya mawasiliano, lakini alipokuwa anarejea alishuku mambo sio shwari.

Inadaiwa dereva huyo ambaye hadi jana ilikuwa haijulikani alikuwa akiwasafirisha wahamiaji hao kwenda Afrika Kusini kupitia mikoa gani ya Tanzania, alitoroka kutoka eneo la tukio kwa usafiri wa pikipiki na kuondoka pia na funguo za gari.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini njia tatu ambazo hutumika kusafirisha wahamiaji haramu kuwa ni kutoka Njiapanda ya Himo au Chekereni kwenda Morogoro na baadaye mikoa ya Iringa na Mbeya hadi eneo la Tunduma.

Njia nyingine inayotumiwa ni ile ya kutoka Njiapanda ya Himo kwenda Muheza kupitia Barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam na baadaye Morogoro hadi Mbeya na njia nyingine ni kupitia Barabara ya Bwawa la kuzalisha Nyumba ya Mungu.


Wimbi la ‘Mashangingi’ kusafirisha wahamiaji

Machi 25, 2024 gari lingine linalofanana na hilo kimuundo, lilikamatwa katika kizuizi eneo la Minjingu wilaya ya Babati, likiwa na wahamiaji haramu 20 kutoka Ethiopia, huku dereva akipeperusha bendera ya CCM ili kuwahadaa polisi.

Uchunguzi wa vyombo vya usalama ulithibitisha gari hilo si mali ya CCM, bali dereva wa gari hilo ambaye ni mkazi wa Dodoma, inadaiwa alifanya hivyo ili lionekane ni gari la kiongozi wa CCM na Polisi wasilitilie shaka.

Aprili 9 mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Manyara lilifanikiwa kukamata gari lingiine la kifahari aina ya Toyota Landcruicer VXR V8 likiwa limebandikwa namba ya serikali likisafirisha wahamiaji haramu 17 nao wakiwa ni raia wa Ethiopia.

Shangingi hilo lilibainika likiwa namba nyingine za magari binafsi ambayo ndiyo halali na lilikamatwa katika Kijiji cha Kiongozi, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, ikiwa ni mbinu ya kuwakweka polisi na maofisa uhamiaji.

Machi 23, mwaka huu, gari lingine aina ya Toyota Land Cruiser VXR V8 lililokuwa linapeperusha bendera ya CCM, nalo lilikamatwa likiwa na wahamiaji haramu 20 raia wa Ethiopia katika kizuizi cha Minjingu, wilayani Babati mkoani Manyara.