Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafugaji wapewa mbinu kuwapa urithi wa elimu watoto

Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise (katikati) akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya kidato cha sita ya Shule ya Sekondari Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kushoto ni Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Laizer na kulia ni Mkuu wa shule hiyo William Ombay. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Kutokana na asilimia kubwa ya wafugaji nchini kupenda kutoa urithi wa mifugo kwa watoto wao, wametakiwa kubadilika na kuwapa urithi wa elimu watoto wao .

Simanjiro. Jamii ya wafugaji imetakiwa kuwapatia urithi wa elimu watoto wao ili miaka ijayo waweze kujitegemea na kuhudumia watu kupitia elimu waliyoipata na siyo kuwarithisha mifugo pekee.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd, Onesmo Mbise ameyasema hayo kwenye mahafali ya kwanza ya wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Naisinyai wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mbise amesema pamoja na kuwa na mifugo, wafugaji wakiwapatia elimu watoto wao watakuwa na manufaa makubwa zaidi kwani wataweza kufanya mambo makubwa kupitia elimu.

Amewapongeza wahitimu hao kwa kufanikiwa kupata elimu ya kidato cha sita hivyo wanasubiri kufanya mitihani na kujiunga na vyuo mbalimbali kisha waanze kuwatumikia Watanzania.

“Nawapongeza ninyi wanafunzi kwa kuhitimu kidato cha sita kwani miaka ijayo mtakuwa watu fulani muhimu kwenye jamii kupitia elimu mliyonayo hivi sasa,” amesema Mbise.

Hata hivyo, amewatakia heri ya kufaulu mtihani wanafunzi wote 33 katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita wanayotarajia kufanya mwanzo mwa mwezi Mei mwaka huu.

Mkuu wa shule ya sekondari Naisinyai William Ombay amemshukuru Mbise kwa kupitia kampuni yake kuahidi kukamilisha baadhi ya changamoto zinazowakabili.

“Pamoja na yote, tunashukuru kwa ahadi zako kuwa suala la ukosefu wa umeme kwenye bweni la wasichana umelibeba, na pia visima vya kuhifadhi maji,” amesema Mwalimu Ombay.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa kidato cha sita, Joseph Emmanuel amesema shule hiyo imeanzishwa mwaka 2006 ikiwa ya kidato cha kwanza hadi cha nne na mwaka 2021 ikapanda hadhi na kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.

Emmanuel amesema wanafunzi 53 walipangiwa kuanza kidato cha tano, kati yao wanafunzi 40 wakaripoti ila wakapungua kwa wengine saba kuhama na kubakia wanafunzi 33.

Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amesema watampa ushirikiano wa kutosha mwekezaji mzawa Onesmo Mbise kupitia Kampuni ya Franone Mining LTD inayochimba madini ya Tanzanite.

“Hii ni hatua nzuri ya mahusiano mema ya uwekezaji kupitia kampuni yako ya Franone Mining LTD na jamii ya Kata ya Naisinyai, tunatarajia tutashirikiana vyema,” amesema Taiko.