Waeleza jinsi miradi ya TASAF ilivyoboresha maisha

Muktasari:

  • Mtindo wa kuwamilikisha wananchi miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), umeelezwa kuleta tija na uwajibikaji katika miradi hiyo.

Rufiji. Baadhi ya watendaji na wananchi wilayani Rufiji Mkoa Pwani wameeleza mafanikio waliyopata kwa uwezeshaji waliopata kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wakisema imeboresha maisha yao.

 Wameyasema hayo juzi Mei 31 wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya TASAF katika maeneo ya Utete na Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji.

Ziara hiyo ya siku mbili katika Mkoa wa Pwani ilihusisha viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, wakifuatana na Kamati ya Usimamizi ya Jumuiya ya TASAF kutoka Kizimkazi-Dimbani na Wilaya ya Rufiji.

Mchuuzi katika soko la Utete, Zawadi Said ameishukuru TASAF kwa kuboresha soko hilo la kijiji na kujenga shule ya sekondari ya wasichana jirani iliyopewa jina la Samia Suluhu Hassan.

"Soko la zamani halikuwa katika hali nzuri, lilikuwa bovu na chafu kila mahali. Ilikuwa ngumu kufanya biashara, hasa wakati wa mvua," alibainisha Saidi.

Soko hilo limejengewa mabanda 82, kibanda tofauti cha samaki chenye mabanda manne, bucha, vyoo sita na shimo moja la watu wenye mahitaji maalum.

Pia limejengwa duka, ofisi, eneo la taka na tanki la kuhifadhi maji.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Utete, Edmund Karugira aliomba eneo la kuuzia samaki liongezwe ili kuwezesha wafanyabiashara wengi wa samaki kuuza bidhaa zao.

Soko hilo lililozinduliwa Aprili mwaka huu limejengwa kwa zaidi ya Sh174.3 milioni na kati ya hizo zaidi ya Sh125.6 milioni zilitokana na TASAF, Sh46 milioni kutoka vyanzo vya ndani vya mapato ya halmashauri na Sh2.7 milioni kutoka kwa jumuiya zinazofaidika.

Akizungumzia miradi hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rachel Chuwa ameeleza kuwa Serikali inatumia mbinu ya kutoka chini kwenda juu katika kuanzisha na kutekeleza miradi ya jamii.

"Hiyo inawapa watu hisia ya umiliki, inakuwa rahisi kwao kushiriki na kusaidia utekelezwaji wa miradi hiyo," amesema Chuwa.

Alisema kumekuwa na ushirikiano kati ya jamii husika, TASAF na mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuwamilikisha wananchi miradi inayojengwa. 

"Mradi utakapokamilika, kuna uwezekano mkubwa wa jamii kuulinda na kuudumisha uwepo wake kwa vile ni mradi wao, si wa TASAF pekee au wa Serikali," amesema.

Kwa upande mwingine mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Miradi ya TASAF katika Kijiji cha Kizimkazi-Dimbani Zanzibar, Mussa Ally amebainisha kuwa Tanzania bara na visiwani zinakabiliwa na changamoto zinazofanana, kuanzia mahitaji ya jamii hadi utekelezaji wa mradi mbalimbali.

“Imekuwa ni safari ya kutufungua akili, tukaja kubaini ni nini kinasababisha kutoshirikishwa kwa jamii, na pia tukagundua sio tatizo la Zanzibar pekee, lakini sasa tunajua nini kifanyike kutatua hilo.

"Kazi ya jamii inahitaji kujitolea; changamoto haziepukiki; hili ndilo tunalochukua kutokana na uzoefu wa wenzetu hapa Rufiji," amesema.