Wadau wataka uwekezaji kwenye miundombinu ya nishati

Arusha. Uwekezaji katika miundombinu ya sekta ya nishati umetajwa kuwa nyenzo ya kuyafikia maendeleo endelevu nchini na Afrika Mashariki.
Kauli hiyo inakuja, katikati ya jitihada za Afrika kuhakikisha inawaunganishia huduma ya umeme wakazi wake milioni 300 ifikapo 2030, kati ya milioni 600 waliopo gizani sasa.
Katika kulifikia hilo, mataifa 14 katika bara hilo yamesaini mikataba ya utekelezaji wa azimio hilo, huku yakikubaliana umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kufanikisha safari hiyo.
Wito wa umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya nishati, umetolewa leo, Ijumaa Januari 31, 2025 na Makamu wa Rais, Nishati na Miundombinu, Stanbic Bank, Joe Mwakanjuki katika Mkutano wa tano wa Ushirikiano wa Nishati Afrika Mashariki (EA-ECS) 2025, jijini Arusha,
Amesema kadri Afrika Mashariki inavyoelekea katika zama mpya za mageuzi ya sekta ya nishati, Tanzania inachukua nafasi muhimu kuunda mustakabali wa sekta hiyo.
Ameeleza ni muhimu uwekezaji katika miundombinu ya nishati ili kuchochea maendeleo endelevu ukazingatiwa.

Kwa mujibu wa Mwakanjuki, benki imekuwa ikiwezesha uwekezaji, katika miundombinu na kusaidia maendeleo ya viwanda kama vichocheo vya ukuaji uchumi.
Katika mkutano huo wa siku mbili, kauli mbiu ni "kuwezesha Afrika Mashariki, kufungua uwezo wa nishati wa Tanzania kwa soko la likanda,”
Viongozi wa Serikali, wawekezaji na wataalamu wa sekta ya nishati ni makundi yaliyokutana kujadili suluhisho la kupanua upatikanaji wa nishati, kuunganisha vyanzo vyake na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Sambamba na hayo, Mwakanjuki amesema wanatambua umuhimu wa uwezeshaji wa kifedha katika kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya nishati.
"Kwa kutumia utaalamu wa Standard Bank Group, Stanbic imekuwa na mchango mkubwa katika kubuni suluhu za kifedha zinazopunguza hatari katika uwekezaji, kuwezesha ushirikiano wa kimkakati na kuharakisha maendeleo ya miradi mikubwa ya miundombinu," amesema.
Amesema benki hiyo imechangia katika miradi mikubwa ya nishati ikiwemo utafiti wa uchumi mkuu wa gesi asilia (LNG) nchini.
“Kushiriki kwa Benki ya Stanbic katika EA-ECS 2025 kunadhihirisha dhamira yetu ya kusaidia ukuaji wa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo," amesema.