Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau waipinga kauli ya Waziri Simbachawene

Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora, George Simbachawene akizungumza na wakuu wa taasisi za umma Jijini Dodoma leo Machi 3, 2025

Muktasari:

  • Kauli za wadau zimekuja baada ya jana Jumatatu Machi 3, 2025 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kuwataka wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kutumia hekima na busara kushughulikia masuala ya watumishi ikiwamo uhamisho, kupanda madaraja na mishahara


Dar es Salaam. Wadau wa utumishi wa umma wametaka uamuzi kuhusu masuala ya utumishi ufuate kanuni, sheria na mfumo stahiki badala ya utashi wa kiongozi wa taasisi au shirika husika. 

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 4, 2025 wamesema kutofuatwa kwa hatua hiyo kunasababisha urasimu, maombi ya uhamisho kukaa muda mrefu au watumishi kutopandishwa madaraja. 

Baadhi ya wakuu wa taasisi za umma wakimsikiliza waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora George Simbachawene (hayupo pichani) kwenye kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma leo Machi 3, 2025

Kauli zao zimekuja baada ya jana Jumatatu Machi 3, 2025 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kuwataka wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kutumia hekima na busara kushughulikia masuala ya watumishi ikiwamo uhamisho, kupanda madaraja na mishahara.

Simbachawene alieleza hayo wakati akifungua kikao kazi na wakuu wa taasisi za umma, jijini Dodoma akisema wapo watumishi wa umma, kila wanapojaribu kuomba kuhamishiwa walipo wenza wao, wakuu wa taasisi za umma hawashughulikii. 

Waziri alisema wapo watumishi waliokaa miaka 20 ya ndoa, lakini hawakuwahi kupata nafasi ya kuishi zaidi ya mwezi mmoja wa likizo na wenza wao. 

“Jibu lenu ninyi huwa ni rahisi tu, tumepeleka sijui utumishi. Wale watu wakipata nafasi wanakuja kujaa pale ofisini kwangu wakiulizia barua ya uhamisho, imekwama utumishi. Nani kakwambia ofisa utumishi, lakini ofisa utumishi barua ameiweka ofisi kwake hataki kuipeleka,” alisema Simbachawene. 

Katika maelezo yake, alisema analizungumza hilo la uhamisho kwa sababu, mbali na uongozi, yeye ni baba na babu na anaona hasara ya wenza wanapoishi tofauti na hata watoto wanapoishi mbali na wazazi.

“Mimi nitabaki na hoja yangu hii kwa kuwa sina namna ya kufanya. Siwezi kutumia nguvu, siwezi kuwaamrisha. Mimi narudia kuwaomba, tumieni busara katika eneo hili,” alisema.

Baadhi ya wakuu wa taasisi za umma wakimsikiliza waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora George Simbachawene (hayupo pichani) kwenye kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma leo Machi 3, 2025

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Henry Mkunda amesema kinachoonekana ni matumizi zaidi ya utashi wa mtu (kiongozi) kuliko kufuata sera, kanuni na taratibu au mifumo iliyowekwa. 

Kutokana na hilo, Tucta imeshauri Serikali kutumia zaidi mifumo na sheria zilizowekwa na isimamie utekelezaji wa sera hizo badala kutoa nafasi ya kutumia utashi wa mtu,  binafsi akisema siyo njia nzuri katika utumishi wa umma. 

“Ni vizuri sheria, kanuni na mifumo iliyopo izingatiwe badala ya kutegemea utashi wa mtu binafsi,” amesema Mkunda.

Hata hivyo, Mkunda amemshukuru Simbachawene kwa kuzungumza hadharani masuala hayo, akisema kama kiongozi huyo ameyasema hadharani maana yake mambo hayo yapo. 

“Kwa mtazamo wangu na kuangalia haraka haraka utagundua kuna upungufu mahali fulani katika suala nzima zima na menejimenti na utumishi wa umma. Kama kuna upungufu huo na sababu inaonekana ubabe na roho mbaya…Basi nina wasiwasi na mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu kwenye utumishi wa umma.

“Pamoja na kwamba tunajinasibu tuna mifumo imara ya utumishi wa umma, lakini bado inaonekana tuna taratibu zile zile za kutumia mifumo ya kizamani ya usimamizi wa rasilimali watu kuanzia ngazi ya juu hadi chini,” amesema.

Mkunda, kwa nyakati tofauti Tucta imekuwa ikilalamikia masuala hayo katika majukwaa mbalimbali ikiwamo kuandika barua kwenda Serikalini. 

“Tulishawahi, kuandika hata katika Baraza Kuu la Utumishi Serikalini kwamba iwe ni wakati mwafaka sasa watu kurudishwa kukaa na familia zao kwa sababu kuna magonjwa, watu hukaimu muda mrefu. Katika majukwaa mbalimbali tumekuwa tukisisitiza haki itendeke kwa watumishi. 

Kuhusu madai ya ndoa feki, Mkunda amesema hana uhakika wala ushahidi wa hilo, ingawa inapotokea mtu akanyimwa nafasi kwa kigezo cha ndoa basi anafanya lolote ikiwamo kughushi ili apate anachokihitaji. 

“Ninachojua sasa hivi mfumo ulivyo ndoa nyingi zinasajiliwa na Rita (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini), hivyo ni rahisi kubaini hilo na Rita watakuwa na uhakika wanachokifanya,” amesema Mkunda. 

Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Ushauri, Habari na Utafiti (RAAWU), Joseph Sayo ameungana na Mkunda akitaka kanuni na sheria zifuatwe katika kutenda haki za watumishi.

 Sayo amesema kinachotakiwa kufanyika ni mamlaka husika kuyafanyia kazi maombi yote kwa mujibu wa utaratibu na kanuni zilizopo siyo kwa utashi kiongozi wa ngazi husika au taasisi. 

“Utashi wa mtu uondolewe na taratibu zifuatwe katika utendaji kazi badala ya kutegemea utashi wa kiongozi,”amesema Sayo huku akisema alichokisema Simbachawene ndicho kilichopo. 

“Mfano mume anafanya kazi serikalini, lakini mke yupo sekta binafsi linapokuja suala la uhamisho, changamoto inakuja katika zile fomu za sekta ya umma za kuomba uhamisho zinahusu watumishi wa umma kwa umma siyo sekta binafsi,”

“Kuna wafanyakazi walishanipigia simu wakilalamikia suala hilo kwamba wenzao wapo sekta binafsi wanataka wawafuate, lakini katika fomu wanatakiwa waonyesha namba za wenza wao ambazo katika sekta binafsi hazipo,”amesema Sayo.

Sayo amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya watumishi kukaimu muda mrefu, licha ya sheria kueleza watu wanatakiwa wakae nafasi kwa miezi sita, kisha kuthibitishwa au kutafutwa mwingine. 

“Urasimu umekuwa ni mkubwa, taasisi zinapeleka majina utumishi lakini wanajibiwa kuwa kuna upembuzi unafanyika, ndiyo maana watu wanakaimu muda mrefu kuna changamoto kubwa naungana na Simbachawene suala hili liondolewe.”

Rais wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alikuwa na maoni tofauti akisema matatizo hayo yamekuwa kwa muda mrefu huku akimshangaa Simbachawene kulalamika. 

“Nilitarajia Simbachawene atasema Serikali imewachukulia hatua watu waliobainika kunyima haki za watumishi wanaonyima haki za uhamisho au kutopandisha madaraja, lakini yeye analalamika, sasa kazi yake ni nini,” amehoji Mukoba.