Wadau elimu walaani mwanafunzi aliyefariki akitekeleza adhabu ya mwalimu

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage

Muktasari:

  • Mwanafunzi Gloria Faustine (14) alifariki Machi 17, 2023 wakati akitekeleza adhabu aliyopewa na mwalimu wake ya kuchimba kifusi kwa kosa la kuzungumza lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza akiwa katika mazingira ya shule.

Dar es Salaam. Taasisi ya HakiElimu imelaani kitendo cha mwanafunzi Gloria Faustine (14) kupewa adhabu iliyosababisha kifo chake na kutoa wito kwa Serikali kuhakikisha dhana ya adhabu chanya inapewa mkazo katika mafunzo tarajali na kazini kwa walimu.

Tukio hilo lilitokea Machi 17, katika shule ya Sekondari Mwinuko, iliyoko Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, jijini Mwanza ambapo mwanafunzi huyo alikuwa akitekeleza adhabu aliyopewa pamoja na wenzake kwa kosa la kuzungumza lugha ya Kiswahili katika mazingira ya shule.

Wakati akitekeleza adhabu hiyo ya kuchimba kifusi yeye pamoja na wenzake 30, Gloria aliangukiwa na jiwe jambo ambalo lilisababisha kukatisha uhai wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage amesema dhana ya adhabu chanya ikitiliwa mkazo katika mafunzo ya walimu itasaidia kuepukana na matumizi ya adhabu ya kikatili.

“Wakati wa mafunzo kwa vitendo kwa walimu utoaji wa adhabu unaweza kuwa moja ya tathmini, hivyo tunaendelea kusisitiza matumizi ya adhabu chanya na vichocheo chanya katika kuimarisha nidhamu na kujifunza,” amesema.

Pia ametoa rai kwa Serikali kurejea upya mapendekezo yanayotolewa na wadau kuhusu matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia ngazi ya sekondari..

Ameongeza na kusema ni wazi kuwa watoto wanaotoka shule za msingi na hasa za umma kuingia kidato cha kwanza, wanakuwa hawajawa tayari kuweza kutumia lugha ya Kiingereza katika kuzungumza na kujifunza.

“Kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari, itatoa fursa kwa watoto kujifunza kwa ufasaha na kufundishwa vyema Kiingereza na lugha nyingine kama lugha za kigeni,” amesema.