Wachimbaji madini wawili wafariki mgodini

Muktasari:
- Wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, wamefariki dunia kwa kukosa hewa baada ya kuingia kwenye mgodi ambao hautumiki kwa sasa.
Mirerani. Wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, wamefariki dunia kwa kukosa hewa baada ya kuingia kwenye mgodi ambao hautumiki kwa sasa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Mareson Mwakyoma amesema tukio hilo limetokea leo Jumatano Mei 26, 2021 saa 5 asubuhi.
Kamanda Mwakyoma amesema wachimbaji hao waliingia kwenye mgodi huo wa kampuni ya Kilimanjaro Mining unaomilikiwa na mfanyabiashara wa jijini Arusha, Alhakim Mulla.
Amewataja waliokufa kuwa ni Omary Shabani (44) mkazi wa Kazamoyo Mirerani na Frank Ndekirwa (43) mkazi wa Tengeru mkoani Arusha.
"Chanzo cha vifo hivyo ni wachimbaji hao kuingia kwenye mgodi huo ambao hautumiki wakakosa hewa na kufariki dunia," amesema kamanda Mwakyoma.