Wabunifu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wapewa Sh107 milioni

Dar es Salaam. Wajasiriamali wanne wa mazingira nchini Tanzania wamepokea jumla ya Sh107 milioni (€40,000) kama ruzuku ya kuendeleza bunifu zao zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii zilizo hatarini zaidi.
Tuzo hizo zilitolewa na Climate-KIC kwa kushirikiana na kampuni ya ubunifu ya SmartLab, kupitia programu ya Adaptation & Resilience ClimAccelerator 2025, baada ya mashindano ya Demo Day yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Washindi hao ni Rada 360, Mbegu Nzuri Biotech Farms, InsectUp, na HERVEG.05, kila mmoja akipokea kiasi cha €10,000 (takribani Sh26.7 milioni) ili kusaidia utekelezaji wa suluhisho zao za kimazingira.
Programu hiyo ilianza kwa kupokea zaidi ya maombi 170 kutoka kwa wajasiriamali waliotokea mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Iringa, Arusha, Dodoma, Zanzibar, Mwanza, na Singida.
Baada ya mchujo mkali, wajasiriamali 10 walichaguliwa kushiriki katika mafunzo ya kina na kupata usaidizi wa kitaalamu, rasilimali, na fursa ya kushirikiana na wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Wajasiriamali hao walikuwa ni Tanzania Viable Farms, HERVEG.05, NDUGUNAMITI ENTERPRISES LTD, Kilimomax Solutions, InsectUp, Rada 360 Limited, THORNTSORN, Kesho Technologies Company Limited, DMA na Addrone Digital
Katika siku ya maonyesho ya mwisho Demo Day iliyofanyika Alhamisi, Aprili 3, 2025, kila mshiriki alipata fursa ya kuwasilisha na kujinadi mbele ya wageni waalikwa, wawekezaji na majaji waliobainisha ubunifu wenye athari kubwa kwa jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Sophie White, Meneja Mwandamizi wa Programu, Ubunifu na Masoko Yanayoibukia Climate-KIC, alisema: “Kupitia ClimAccelerator, tumetoa maarifa na zana muhimu kwa wajasiriamali hawa, kuwasaidia kupima ubora wa suluhisho zao na kuzijaribu katika mazingira halisi. Tunaamini wanaweza kuleta mabadiliko chanya mijini na vijijini.”
Laurian Mafuru, Mratibu wa Programu kutoka SmartLab, aliongeza: “Tunahimiza suluhisho hizi zijaribiwe zaidi katika mazingira halisi ili kuthibitisha ufanisi wake na kuboresha zaidi bunifu zao. Lengo ni kuona mabadiliko endelevu katika maeneo yaliyoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.”
Washindi
Rada 360: Inatumia teknolojia ya anga kama vile setelaiti, uchunguzi wa Dunia, na elimu ya anga kutoa taarifa sahihi kwa wakulima kuhusu hali ya udongo na hali ya hewa, na hivyo kuboresha mbinu za kilimo.
Mbegu Nzuri Biotech Farms: Hutoa mbegu bora zenye ustahimilivu kwa mabadiliko ya hali ya hewa, zikiwa ni msaada mkubwa kwa wakulima wanaokabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
InsectUp: Inatumia nzi aina ya Black Soldier Fly kubadilisha taka za kikaboni kuwa chakula cha mifugo na mbolea bora, hivyo kuchangia katika kilimo endelevu na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
HERVEG.05: Inalenga kupambana na utapiamlo vijijini kwa kuwapatia wanawake wakulima vifurushi vya mboga zenye virutubisho na kuku, sambamba na kutoa mafunzo na mikopo ya kidijitali kupitia simu.