Wabunge, vigogo wa zamani CCM wafikishwa mahakamani

Muktasari:
- Waliowahi kuwa wabunge na wenyeviti wa CCM wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tanga wakituhumiwa kwa mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia hasara serikali ya Sh30 bilioni
Tanga. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewafikisha mahakamani wakurugenzi sita wa bodi ya kiwanda cha chai cha Mponde Tea Estate akiwamo mbunge wa zamani wa Bumbuli (CCM), William Shelukindo na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Mbali na Shelukindo aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini wengine ni mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoa wa Mbeya, Nawab Mulla ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa Mbarali, mwenyekiti wa zamani wa CCM wilaya ya Lushoto, Richard Mbughuni, Shahdad Mulla, Richard Semroki na Rajab Msagati.
Imedaiwa mahakamani hapo leo Septemba 27,2018 na mwanasheria wa Serikali, Seth Mkemwa akisaidiana na mwanasheria wa Takukuru, Adam Kilongozi mbele ya hakimu mkazi mfawidhi Mkoa wa Tanga, Desdery Kamugisha kwamba kati ya mwaka 2000 na 2013 washtakiwa hao walihusika na mashtaka hayo kwa nyakati tofauti.
Amedai shtaka la kwanza linalowahusu Shelukindo, Mulla, Shahdad na Mbughuni ni kula njama kwa kuagiza nje ya nchi malighafi ya Sh135 bilioni kwa ajili ya kiwanda cha Mponde pamoja na wakulima wa chai na kisha kudai msamaha wa kodi hivyo kuisababishia Serikali hasara ya Sh30 bilioni.
Shtaka la pili, ambalo linawahusu washtakiwa wote sita kwa mujibu wa mwanasheria huyo ni kuisababishia Serikali hasara ya Sh30 bilioni kinyume na aya ya 10 ya jedwali la kwanza la kifungu cha 57(1) na kifungu cha 60 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 pitio la mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho kwa sheria namba 3 ya mwaka 2016.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Rwegasira aliwata washtakiwa hao wanaotetewa na wakili Sweetbert Rwegasira kutojibu chochote kwa sababu mashtaka hayo ni ya mahakama ya makosa ya rushwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 11,2018 itakapotajwa tena na washtakiwa wamepelekwa rumande.