Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waathirika wa ukeketaji, ndoa za utotoni waanika magumu wanayopitia

Mtoto Neema Petro akizungumza na mwandishi wa makala hii, Imani Makongoro

Tarime. Wakati miji ya Sirari na Nyamongo ikitajwa vinara wa ukeketaji wilayani humo na kusababisha athari zaidi ya ndoa za utotoni, waathirika wa ndoa hizo wameeleza magumu wanayopitia, wengine wakidai kutengwa na familia zao.

Wilaya ya Tarime ni miongoni mwa wilaya za mkoa wa Mara unaotajwa kuwa wa tatu kwa ndoa za utotoni nchini, ukiongozwa na Shinyanga, Tabora na Dodoma ni wa nne.

Mtoto Veronica Shedrack ambaye alifukuzwa kwao baada ya kukataa kukeketwa ili aolewe. Picha na Imani Makongoro

Kimataifa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania ilitajwa kuwa ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.

Takwimu hizo zilionyesha Sudan Kusini kiwango cha watoto walio chini ya miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 Uganda  40 na Tanzania ni asilimia 31.

Hapa nchini kwa mujibu wa takwimu za kimataifa kutoka utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) za mwaka 2015/16 zinaonyesha Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa asilimia 59, ukifuatiwa na Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.

Wakizungumza athari walizokabiliana nazo walipotembelewa na msafara wa Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni (Caravan trip) uliofadhiliwa na mashirika ya Msichana Initiative na Plan International, baadhi ya waathirika wa ndoa hizo wilayani Tarime wamedai chanzo cha ni mila za tohara ambayo msimu huu zinatarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu kwa wavulana na wasichana.

Baadhi ya waathirika wanasema kila msimu wa tohara  unapomalizika ndipo kunakuwa na matukio mengi ya ndoa za utotoni, mabinti wengi wakilazimishwa kukatisha masomo ili waozwe.

Sister Jackline Gbanga akizungumza na mwandishi wa makala hii, Imani Makongoro

Diana Mwita (13) sio jina lake halisi anasema alipofika darasa la tatu, mama yake mzazi alitaka aolewe.

"Alikuwa akiniambia, nataka afe kabla hajala mahari yangu, wakati huo alikuwa amekuja kuniposa mwanaume mkubwa zaidi ya baba yangu, nilikataa, nikawa napewa kipigo kila siku," anasema.

Anasema alikimbilia Polisi ndipo mama yake aliyemtaja kwa jina moja la Eliza alikamatwa, lakini akamwambia atakapoachiwa hataki amkute nyumbani, hivyo alikwenda kuomba msaada wa malezi kwenye nyumba salama ya mabinti wanaokimbia ukatili ya ATFGM Masanga, ambako analelewa hapo hadi sasa akijifunza ufundi cherehani.

Binti mwingine, Neema Petro (13) anasema msimu uliopita wa tohara alitakiwa kuwaongoza wasichana wenzake kukeketwa.

"Baba yangu ni mzee wa kimila wa ukoo wa Weregi aliponieleza hivyo nilikataa akawa mkali ikabidi nikubali lakini kwa shingo upande, kabla ya tukio hilo nilikwenda kumshirikisha mchungaji ambaye alinisaidia kutoroka," anasema.

Anasema mdogo wake alibaki na akakeketwa, ingawa alipoteza maisha katika tukio hilo la mwaka 2022. Ambapo alikuwa na  miaka 11 na tangu wakati huo baba yake alimkataa akamwambia atafute mzazi mwingine.

"Sijawahi kurudi nyumbani tangu wakati huo kwani mama aliapa siku nitakayorudi tohara yangu ipo palepale," anasema Neema.

Mkurugenzi wa ATFGM, Sista Jacline Gbanga anasema kuna mabinti kituoni hapo hata kwenda likizo nyumbani kwao ni shida kutokana na wazazi wao kuwalazimisha kuolewa wakiwa wadogo.

"Wapo wazazi wengine huwa wanakuja hapa na kutufanyia vurugu, bahati nzuri tunafanya kazi na ustawi jamii, hivyo hawawezi kumchukua binti mikononi mwetu kirahisi," anasema.

Sista Jackline anasema kinachochochea ndoa za utotoni ni mila mbaya ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike.

Mbusiro Mwita ni shuhuda, anasema mdogo wake Maseke alikatishwa masomo na kuozeshwa kwa mwanaume mtu mzima rika la baba yao.

"Alipitia magumu kwenye ndoa ile hadi alipoamua kutoroka na kuondoka, japo hadi sasa ameshindwa kutimiza ndoto yake ya kuwa nesi," anasema Mbusiro akiiomba jamii ilaani ndoa za utotoni ambazo zinakatisha ndoto nyingi za watoto wa kike.

Veronica Shedrack aliyehitimu kidato cha sita na sasa anasubiri kujiunga na masomo ya elimu ya juu anasema baba yake alikataa kuishi naye kwa sababu hajakeketwa.

"Nilikuwa nimemaliza mitihani ya darasa la tatu nasubiri kuingia la nne, niliona wenzangu waliokuwa wameketwa waliozeshwa na kupewa majukumu ambayo hawakuwa wakiyaweza, ndipo nikatoroka na kukimbilia nyumba salama," amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Peragia Barozi anasema ukeketaji ni chachu ya ndoa za utotoni, kwani jamii nyingi za wilaya hiyo zinaamini mtoto anapotahiriwa au kukeketwa anaonekana ni mkubwa na ametosha kuoa au kuolewa.

"Sina takwimu sahihi ila ndoa za utotoni hapa Tarime zipo japo zinaanza kupungua, miaka ya 1999 ilikuwa wakianza kukeketa, binti akifika darasa la nne analipiwa mahari kabisa na akimaliza la saba anaolewa.”

Anasema wilaya hiyo yenye vijiji 88, inahitaji nguvu ya ziada kutokomeza ndoa hizo kwa kuwapa elimu wazee wa kimila,  kwani baadhi ya vijiji hazifikiwi.

"Ukeketaji ni kichocheo kikubwa cha ndoa hizi hapa Tarime na maeneo hatari zaidi ni yale yaliyopo mpakani kama Sirari na Nyamongo kwa ajili ya madini, hata hivyo tumeweka utaratibu kukomesha matukio hayo.”

"Vilevile uwepo wa mtandao wa kupinga ndoa za utotoni na shule za sekondari za kata vimesaidia kupunguza ndoa hizi," anasema.


‘Ndoa za utotoni ni janga’

Mratibu wa Mtandao wa kupinga Ndoa za Utotoni wenye mashirika 87, Lilian Kimati anasema ndoa za utotoni ni janga.

Anasema kutokana na janga hilo wadau wa mtandao huo ulioanzishwa  mwaka 2012 wakati huo ukiwa na mashirika 12 ulipaza sauti ukitaka yafanyike  mabadiliko ya sheria ya ndoa, ambayo iliruhusu binti anayeanzia miaka 15 kuolewa.

"Tuliipinga hii sheria na kufanya vikao na Serikali na wabunge ili kubadilisha sheria ya ndoa tukiongozwa na mwanachama wetu Rebecca Gyumi, tukaenda mahakamani na kushinda, Serikali ikatakiwa ibadilishe sheria hii lakini bado haijabadilishwa," anasema.

Anasema wakati hayo yakiendelea, Mtandao huo umeendelea kufanya kampeni mbalimbali kupinga ndoa hizo ikiwamo kutoa elimu katika mikoa mbalimbali nchini.

"Safari hii tumeandaa msafara (Caravan trip) kwenye mikoa minne inayoongoza kwa ndoa za utotoni, tukishirikiana kwa karibu na mashirika yetu matano ya Msichana Initiative, Binti Makini, Medea, Plan İnternational na My legacy kutoa elimu," anasema Lilian.

Mtandao huo unapaza sauti kupinga vitendo vya ukatili ikiwamo ndoa za utotoni huku ukitaka sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 na 17 kibadilishwe ili kumaliza janga hilo.

Msimu huu kupitia Caravan trip inakwenda kwenye mikoa ya Mara, Shinyanga, Tabora na Dodoma ambayo inaongoza nchini kuwa na matukio ya ndoa za utotoni.

Lengo ni kutoa elimu katika shule mbalimbali na jamii sanjari na kukutana na viongozi wa maeneo hayo ili kuzungumzia changamoto hizo na namna ya kuzitatua.