Waathirika mafuriko Mbeya wapewa msaada, chakula siku 90

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson (kulia) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera (Katikati) wakipokea misaada ya vitu mbalimbali kutoka kwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera ,Bunge na Uratibu) George Simbachawene (kushoto) kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Kaya ya Uyole Jijini Mbeya .
Muktasari:
- Serikali imetoa msaada mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko ya mvua yaliyotokea Januari 7, 2023, Kata ya Uyole jijini Mbeya huku kuwataka kuchukua tahadhari ikiwemo kutokujenga maeneo yaliyozuiwa.
Mbeya. Serikali imetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko jijini Mbeya ikiwemo magodoro, mikeka, vyombo vya kupikia na chakula kitakachotolewa kwa kipindi cha miezi mitatu (sawa na siku 90).
Msaada huo umekabidhiwa leo Jumatano, Januari 11, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene kwa wakazi wa Kata ya Uyole ambao wameaathiriwa na mafuriko ya mvua yaliyotokea Januari 7 mwaka huu na kuziacha kaya zaidi ya 20 zikiwa hazina makazi.
Waziri Simbachawene ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera na Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Dk Tulia Ackson.
Viti ambayo vimekabidhiwa ni tani 50 za mahindi, magodoro 300, mablanketi 1,200, mikeka 550, madumu ya maji 600, sufuria, vikombe, sahani za ndani.
Akizungumza na wananchi hao, Waziri Simbachawene,”nimefika hapa kwa niaba ya ofisi ya waziri mkuu na pia kuna maelekezo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameyatoa katika Jiji la Mbeya ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu na kuhakikisha kwa kipindi cha miezi mitatu waathirika wa mafuriko wanapata chakula.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuwahudumia huku akiwatahadharisha kuepuka kujenga makazi katika maeneo ambayo sio rasmi na ni hatarishi.
“Niwatake tu wale ambao wanajenga kwenye maeneo hatarishi ikiwepo kwenye mikondo ya maji na mabondeni kuchukua tahadhari kwa kuzingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),” amesema Homera.
Naye Dk Tulia ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka katika kuwasaidia wananchi wake huku akisisitiza kuomba kwa upekee jimbo la Mbeya kukumbukwa kutokana na kuwepo kwa changamoto za miundombinu.
“Niombe Serikali kulikumbuka Jimbo la Mbeya kwani changamoto ni nyingi sana zinazohusu miundombinu licha ya kutokea janga hili la mafuriko katika baadhi ya kata jijini hapa.” amesema.