Dar es Salaam. Serikali imesema imepokea migogoro 28,773 ya wanandoa kati ya Julai, 2022 na Aprili mwaka huu, huku Wizara ya Maendeleo ya Jamii ikitaja vyanzo sita vinavyochangia hali hiyo.
Kati ya migogoro hiyo, 22,844 ilisuluhishwa, huku 5,929 ikikosa usuluhishi, licha ya kukatiwa rufaa ngazi ya Mahakama.
Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alisema hayo jana alipofungua kongamano la kwanza la kutafuta suluhisho la kukithiri kwa talaka nchini, lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Waziri alizitaja sababu hizo kuwa ni mawasiliano hafifu ya wanandoa, hali ya kipato, wanandoa kutofahamu wajibu wao, mila na desturi zisizofaa, udhaifu wa malezi kwa watoto na taarifa zisizokuwa na uthibitisho.
Takwimu hizo zinamaanisha kwamba, Serikali kupitia madawati yake ya jinsia ilipokea wastani wa migogoro 106 kila siku katika kipindi hicho, sawa na migogoro minne kila baada ya saa moja.
Dk Gwajima alisema kutokana na migogoro hiyo, watoto 18,922 waliathiriwa katika malezi, baadhi wakikimbilia mitaani, kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya au ndoa za utotoni.
Alishauri vijana kutumia vigezo vya ndani katika uchaguzi wa mke au mume badala ya kutumia mwonekano wa nje.
“Kwanza ni tatizo la mawasiliano hafifu ya wanandoa. Kuna watu wanaamka asubuhi hawaongei, hawaulizani jana ilikuwaje na hakuna vikao vya familia. Kwa hiyo, mshikamano unaanza kupotea,” alisema Dk Gwajima.
Kuhusu tatizo la taarifa alisema|: “Anasikia tu shemeji yako kasema hivi, baba yako kasema hivi, hawakai wakazungumza. Mwingine hasikilizi la mume, la mke anachukua huko barabarani, kwa hiyo shetani anapata upenyo hapo na kuvuruga ukoo wote, ndoa inaondoka.”
Waziri alisema hali ya kipato inaweza kuchangia mgogoro kwa wanandoa walio masikini na hata matajiri, akisema: “Wakati mwingine hata kwa matajiri ndoa zinavunjika, pesa inakuwepo na isilete amani.”
Amesema kwa wanandoa kutofahamu wajibu wao kila mmoja kunachangia migogoro kwenye ndoa.
“Wengi hawazingatii wajibu wao, kila mmoja hajui anatakiwa afanye nini, au tupeane mitihani kabla ya kuingia kwenye ndoa? Mtu anaweza kuwa na vyeti vingi vya elimu lakini hajui wajibu wake wa ndoa ni nini. Ndani ya wiki mbili ndoa imevunjika na tulichangishwa kweli, inaumiza sana kwa kweli,” amesema.
Amesema baadhi ya jamii huedekeza mila na desturi zisizofaa, huku pia kuwapo udhaifu wa malezi ya watoto ambao ni wanandoa wa baadaye.
Bakwata
Kwa upande wake, Naibu Kadhi wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko aliomba wataalamu kusaidia maswali yaliyopo kwenye mkwamo wa wanandoa, akitaja kuwa, je, watu kuishi kwa kuonjana onjana ni tatizo? Je, tunakosea wapi katika namna ya kumtafuta mchumba? na je, send-off ni mbadala wa unyago?
Sheikh Ngeruko alisema wameamua kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo kwa kuwa hupokea maombi ya wanandoa wengi wanaohitaji kuvunja ndoa baada ya kuamua kujitenga, huku wakikosa majibu ya kiini chake.
“Dunia imebadilika, wanapendeza sana kwa teknolojia ya kutengeneza sura, maumbile. Je, si sababu pia ya migogoro kwenye ndoa? Kwa hiyo wataalamu watatuambia namna gani tufanye,” amesema.
Sheikh wa Wilaya ya Ilala, Adam Mwinyipingu alisema kwa asili ya mwanadamu, kupenda ni kazi ya mwanamume na hana sababu yoyote katika upendo huo.
Alisema mwanamke akipenda basi atakuwa amejipendekeza kwa sababu maalumu zilizomshawishi.
“Mwanamke akipenda ni kujipendekeza tu. Sisi wanaume ndiyo chanzo cha furaha katika uhusiano. Ili mwanamume awe mume bora anatakiwa kuwa na sifa sita na mwanamke kuwa mke bora, anatakiwa kuwa na sifa 13,” alisema Sheikh Mwinyipingu bila kuzitaja sifa hizo.
Sheikh Mohamad Iddy, akitoa mada kuhusu maisha ya ndoa na talaka, alishauri jamii kurejesha watoto katika misingi ya malezi ya dini kwa ajili ya kumjengea hofu ya Mungu kabla ya kuingia kwenye ndoa.