Viwanda vya dawa Mloganzila kuajiri maelfu
Mbunge wa Kibamba ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki akimkaribisha Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
Muktasari:
- Wawekezaji kutoka China, Ujerumani wameahidi ajira zaidi kwa Watanzania huku Serikali ikitoa maelekezo kwa Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha dawa zote zitakazozalishwa nchini haziagizwi tena nje ya nchi.
Dar es Salaam. Serikali imeanza rasmi safari ya kujenga kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzila kwa kutumia mfumo wa kisasa unaofahamika kama kongani, ambao unatarajiwa si tu kupunguza gharama za uzalishaji, bali pia kuzalisha maelfu ya ajira.
Mradi huo unaotekelezwa katika eneo la ekari 400 lililopo Mloganzila wilayani Ubungo, Dar es Salaam, unatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 15 kwa kuanzia huku wawekezaji wakubwa kutoka China na Ujerumani wakitangaza kuanza ujenzi wa viwanda vya kisasa vya dawa na vifaa tiba.
Akizungumza leo Ijumaa Mei 8, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema mfumo wa kongani utaiwezesha Tanzania kuondoka katika utegemezi wa dawa kutoka nje kwenda kwenye uzalishaji wa ndani wenye ushindani wa kimataifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari akizungumza katika hafla hiyo kuhusu uwekezaji huo.
“Leo tunaanzisha safari mpya kutoka utegemezi kwenda uzalishaji wa ndani, kutoka kuwa soko la bidhaa za wengine kwenda kwenye viwanda vyetu wenyewe,” amesema.
Mchengerwa amesema mfumo huo utaiwezesha Serikali kuunganisha viwanda, maabara, teknolojia, taasisi za utafiti, mafunzo pamoja na mifumo ya ugavi katika eneo moja maalumu ili kupunguza gharama za wawekezaji.
Amesema badala ya kila kiwanda kujenga miundombinu yake pekee, kutakuwa na matumizi ya pamoja ya maabara za ubora, mifumo ya maji taka, maghala, mifumo ya usalama wa moto na huduma nyingine muhimu.
Akizungumzia maendeleo ya rasilimali watu katika sekta ya afya na viwanda vya dawa, Waziri huyo amesema Serikali itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) ili kuhakikisha kongani ya viwanda vya dawa ya Mloganzila inakuwa kitovu cha elimu, utafiti na ubunifu wa teknolojia za afya nchini.
Amesema Muhas itakuwa mshirika muhimu katika kutoa mafunzo ya wataalamu wa sekta ya dawa, kufanya tafiti za kisayansi pamoja na kuendeleza maeneo ya dawa na kada ya famasia yanayohitajika katika uzalishaji wa dawa za kisasa.
Baadhi ya wananachi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kongani ya viwanda vya dawa na vifaa tiba katika eneo la Mloganzila kwa kutumia mfumo wa kisasa unaofahamika kama kongani.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha Mloganzila inakuwa darasa la vitendo, ambapo wanafunzi hawatajifunza kwa nadharia pekee, bali watapata nafasi ya kujifunza moja kwa moja ndani ya viwanda na maabara za kisasa,” amesema.
Mchengerwa amesema, hatua hiyo itasaidia kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya viwanda vya ndani huku ikiwezesha viwanda hivyo kupata rasilimali watu iliyofundishwa na kuandaliwa hapa nchini badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje.
Mbunge wa Kibamba ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema uwekezaji huo utafungua fursa kubwa za ajira kwa wakazi wa maeneo ya Kibamba, Kwembe na Ubungo.
Mwakilishi wa wawekezaji wa viwanda vya dawa na chanjo kutoka Ujerumani, Peter Hook akizungumza wakati wa hafla hiyo. Zaidi ya wawekezaji 76 wanaozalisha chanjo, dawa, vifaatiba na vitendanishi duniani wamejitokeza kuwekeza Tanzania.
Amelitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuhakikisha eneo hilo linakuwa na mawasiliano ya uhakika kwa ajili ya shughuli za viwanda na teknolojia.
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema tayari wawekezaji wengi wameanza kujitokeza kuwekeza katika viwanda vya dawa kutokana na mazingira yanayowekwa na Serikali.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari amesema Serikali imeanza na kongani mbili ambazo ni Mloganzila yenye ekari 400 na Kibaha yenye ekari 100.
Amesema maeneo hayo yamechaguliwa kimkakati kutokana na ukaribu wake na taasisi za elimu, afya na utafiti.
“Mloganzila ina nafasi ya kipekee kwa sababu ipo karibu na taasisi kubwa za elimu, utafiti na huduma za afya. Tunataka wanafunzi wajifunze kwa vitendo na viwanda vipate wataalamu wanaozalishwa hapa nchini,” amesema.
Amesema Serikali pia imepatiwa ekari 1,000 Bagamoyo kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji Tanzania (Tiseza) kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa zaidi wa viwanda vya dawa katika siku zijazo.
Mwakilishi wa wawekezaji kutoka China, Miyao Ying Yang amesema kampuni yao imewekeza dola za Marekani 50 milioni na inalenga kuanza uzalishaji ifikapo Mei mwaka ujao.
Amesema mradi huo utazalisha zaidi ya ajira 2,000 na utahusisha viwanda vya dawa za kisasa pamoja na tiba asili.
Mwakilishi wa wawekezaji kutoka Ujerumani, Peter Hook amesema wameamua kuwekeza Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa dawa kwa ukanda wa Afrika na kupunguza changamoto za upatikanaji wa dawa wakati wa majanga ya kimataifa.
“Tunaleta teknolojia, utaalamu na ajira. Tunaamini Tanzania inaweza kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa dawa Afrika,” amesema.