Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu zinazoisukuma MSD kugeukia mifumo ya kisasa

Muktasari:

  • Imeeleza mkakati wake wa kupunguza gharama, kuongeza upatikanaji wa dawa na kukabiliana na mtikisiko wa soko la dunia, uzalishaji wa ndani na mageuzi ya mifumo ya kisasa.

Dar es Salaam. Bohari ya Dawa (MSD) imeanza kutekeleza mageuzi ya kimkakati yanayolenga kuifanya taasisi hiyo kuwa ya kisasa, yenye ufanisi na inayojitegemea zaidi kifedha.

Katika kufanikisha hilo, imeanza kujikita katika matumizi ya nishati mbadala, uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya na kuboresha mifumo ya usambazaji.

Akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema taasisi hiyo imeanza safari ya mageuzi kupitia mradi wa “Green Project” unaolenga kuongeza matumizi ya nishati ya jua katika shughuli zake.

“MSD ya kijani ni mkakati wetu wa kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza matumizi ya nishati mbadala. Tayari tumeshafanya uwekezaji katika maeneo kama Mtwara, Dodoma na Chato, na tunaendelea kupanua zaidi,” amesema Tukai.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai.

Amesema matumizi ya nishati hiyo yatasaidia kupunguza utegemezi wa umeme wa kawaida, kulinda mazingira na kuhakikisha uhifadhi salama wa bidhaa za afya, hasa zile zinazohitaji mnyororo wa baridi.

Mradi huo unaotarajiwa kugharimu jumla ya Sh38.1 bilioni tayari umepokea Sh9.5 bilioni kutoka Global Fund kwa ajili ya awamu ya awali ya usimikaji wa umeme wa jua katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Dar es Salaam, huku hatua ya manunuzi ya mkandarasi ikiendelea.

Tukai amesema uhitaji wa nishati ya uhakika katika uhifadhi wa bidhaa za afya ndiyo sababu kuu iliyochochea kuanzishwa kwake.

“Tunashughulika na bidhaa nyeti zinazohitaji mazingira maalumu ya uhifadhi, ikiwemo dawa na vifaa tiba vinavyohitaji mnyororo wa baridi. Nishati ya uhakika ni jambo la msingi, na hapa ndipo mradi wa ‘Green Project’ unapokuja,” amesema Tukai.

Amefafanua kuwa utegemezi wa umeme wa kawaida umekuwa ukileta changamoto, ikiwemo gharama kubwa za bili na wakati mwingine kukatika kwa umeme, hali inayoweza kuhatarisha ubora wa bidhaa za afya.

“Kupitia nishati ya jua, tunalenga kuwa na mfumo wa uhakika usioathiriwa na mabadiliko ya umeme wa gridi, lakini pia kupunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa,” ameongeza.

Kwa mujibu wa MSD, matumizi ya nishati mbadala si tu yatasaidia kupunguza gharama za kila siku, bali pia yatapunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyochangia uchafuzi wa mazingira, hatua inayokwenda sambamba na ajenda ya taifa na kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkaguzi wa Ndani wa MSD, Jarafi Makoka Matembezi, akijibu baadhi ya maswali ya wahariri

Kwa upande mwingine, uwepo wa nishati ya uhakika utaongeza ufanisi wa mifumo ya Tehama inayotumiwa na MSD, ambayo tayari imefikia asilimia 95 ya matumizi, na ambayo ni muhimu katika kusimamia ugavi wa bidhaa za afya kuanzia hatua ya ununuzi hadi usambazaji.

Mbali na mradi huo, MSD inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika mifumo ya usambazaji na uhifadhi wa bidhaa za afya, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu ya kisasa na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

Tukai amesema taasisi hiyo imefikia matumizi ya Tehama kwa asilimia 95 katika shughuli zake, hatua iliyosaidia kuongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji huduma.

“Tunajenga mfumo wa kisasa unaotumia teknolojia kuanzia hatua ya ununuzi, uhifadhi hadi usambazaji wa bidhaa za afya. Hii inasaidia kuhakikisha hakuna upotevu na huduma zinawafikia wananchi kwa wakati,” amesema.

Mbali na nishati, katika sekta ya uzalishaji, MSD kupitia kampuni yake tanzu ya Medipharm imeanza kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje ya nchi kwa kuwekeza katika viwanda vya ndani.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni uzalishaji wa barakoa katika kiwanda cha Keko, Dar es Salaam, ambapo hadi Desemba 2025 zaidi ya barakoa milioni 9.8 zenye thamani ya Sh5.5 bilioni zilikuwa zimezalishwa na kuuzwa.

Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa.

Vilevile, Tukai amesema kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi, Njombe, kimeanza uzalishaji rasmi mwaka 2024 na tayari kimezalisha zaidi ya vipande milioni 8 vyenye thamani ya Sh2.2 bilioni.

Hatua hizo, kwa mujibu wa MSD, zimechangia kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa kutoka nje ya nchi na kuokoa fedha za kigeni.

Katika hatua nyingine, MSD inaendelea na mpango wa kujenga viwanda vya dawa katika eneo la Zegereni, Kibaha, kupitia ubia na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Pia, MSD imepiga hatua kupitia ufufuaji wa kiwanda cha dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) kilichopo Arusha, ambacho kinatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika upatikanaji wa dawa hizo muhimu.

“Kiwanda cha ARV Arusha kinafufuliwa na tayari kuna uwekezaji unaoendelea. Serikali kupitia Msajili wa Hazina inamiliki asilimia 40, MSD asilimia 30 na mwekezaji asilimia 30. Mitambo inaendelea kufungwa, na tunatoka kwenye mfumo wa dawa za kopo kwenda kwenye ufungashaji wa kisasa wa ‘strips’,” amesema.

Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitakuwa na bodi yake na kitaendeshwa kibiashara ili kuhakikisha kinajiendesha kwa ufanisi na tija.

Hatua hiyo inakwenda sambamba na mabadiliko ya sheria yaliyofanyika mwaka 2024 yaliyoiwezesha MSD kuingia rasmi katika uzalishaji wa bidhaa za afya kupitia kampuni yake tanzu, ambayo tayari inaonesha mafanikio.

“Tunatoa huduma, lakini kwa mtazamo wa kibiashara tunapunguza matumizi na kuongeza vyanzo vya mapato. Ndani ya mwaka huu tunaweza kukaribia soko la shilingi bilioni 700,” amesema Tukai.


Uwekezaji SADC

Tukai amesema Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), licha ya changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano (MoU).

Amesema wakati wa majadiliano kulikuwa na mvutano wa kisiasa, na baadhi ya nchi wanachama bado zinatumia mifumo ya zamani ya dawa, huku Tanzania ikiwa imepiga hatua zaidi kiteknolojia.

“Tulitoa mapendekezo ya kufanya maboresho (reforms), lakini bado kuna changamoto, hasa kwenye mifumo ya fedha na uendeshaji,” amesema.

Ameeleza kuwa Tanzania imepewa jukumu la kuandaa ofisi ya kuratibu shughuli za SADC katika sekta ya afya, huku wizara husika ikiendelea na maandalizi ya kuanzisha ofisi hiyo.

“Tunaamini makubaliano tuliyosaini yataanza kufanya kazi vizuri baada ya mifumo kukamilika,” amesema.

Ameongeza kuwa mkakati mkubwa si biashara pekee, bali pia kuifanya Tanzania kuwa kitovu (hub) cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa hizo katika ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC).

“Dira yetu ni kuona Tanzania inakuwa kitovu cha bidhaa za afya katika ukanda huu. Ndiyo maana tunawekeza katika uzalishaji, teknolojia na miundombinu kwa wakati mmoja,” amesema.


Hali ya uchumi

Katika kukabiliana na changamoto za kimataifa, Tukai amekiri kuwa hali ya uchumi wa dunia imeathiri pia sekta ya bidhaa za afya, ikiwemo usafirishaji na upatikanaji wa baadhi ya bidhaa.

Ametolea mfano bidhaa za uzazi wa mpango (kondomu), akisema kuna uwezekano wa bei kupanda kwa asilimia 20 hadi 30 kutokana na changamoto za uzalishaji na usafirishaji.

“Kwa sasa tuna akiba ya kutosha kwa miezi sita, lakini tunafanya juhudi kuhakikisha upatikanaji unaendelea bila kukwama. Wizara ya Afya iko pamoja nasi kuhakikisha hali inakuwa tulivu,” amesema.

Katika kuboresha usambazaji, MSD pia imebaini changamoto ya uchakavu wa magari yake, ambapo baadhi yamekuwa yakitumika tangu mwaka 2011. Hali hiyo imeongeza gharama za matengenezo na kupunguza ufanisi wa usambazaji.

Takwimu zinaonesha pia mapato ya MSD yameongezeka kwa asilimia 103, kutoka Sh315 bilioni hadi Sh640.5 bilioni, huku upatikanaji wa bidhaa za afya ukiongezeka hadi kufikia zaidi ya asilimia 70 mwaka 2026.

Hata hivyo, Tukai amekiri uwepo wa changamoto katika eneo la takwimu na maoteo ya mahitaji ya dawa, akisema bado kuna mapungufu yanayosababisha baadhi ya dawa kuharibika.

“Ni kweli kuna changamoto ya data, lakini dawa zinazoharibika ni chini ya asilimia moja. Zaidi ya asilimia 95 ya dawa zinatumika kabla ya kuisha muda wake, na zinasaidia kuokoa maisha ya wananchi,” amesisitiza.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, MSD imeboresha mifumo ya ndani, ikiwemo kuanzisha kitengo maalum cha usimamizi wa mikataba ili kuhakikisha uwazi na ufanisi katika ununuzi na usambazaji.

Pia, imeendelea kushirikiana na wataalamu wa ndani, hususan wahandisi wa vifaa tiba (biomedical engineers), ili kuhakikisha mashine zinazotumika katika vituo vya afya zinafanya kazi kwa ufanisi.

“Kila tunaponunua mashine, tunahakikisha kuna wataalamu wa kuisimamia. Serikali pia imewekeza wataalamu katika maeneo mbalimbali kuhakikisha huduma zinakuwa endelevu,” amesema.


Yatoa ufafanuzi


Pia, MSD imefafanua masuala mbalimbali yanayoibua mjadala kwa wananchi, ikiwemo tuhuma za dawa kuharibika, upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na mabadiliko ya mahitaji ya bidhaa za afya, ikisisitiza kuwa changamoto hizo zinadhibitiwa na hazijaathiri kwa kiwango kikubwa utoaji wa huduma.

Akijibu maswali ya wahariri, Mkaguzi wa Ndani wa MSD, Jarafi Makoka Matembezi, amesema kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha dawa kinachoweza kuharibika hakipaswi kuzidi asilimia tano, lakini MSD imefanikiwa kukishusha hadi asilimia mbili.

“Kwa mwaka huu, dawa zilizoharibika ni asilimia 0.9 tu, hazijafika hata asilimia moja. Hii inaonyesha usimamizi mzuri wa rasilimali za dawa,” amesema.

Amefafanua kuwa baadhi ya dawa hulazimika kuhifadhiwa kwa ajili ya dharura, kama za kuumwa na nyoka, hivyo endapo hazitatumika kwa wakati zinaweza kuharibika.

Kwa upande wake, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, amesema mabadiliko ya magonjwa na tiba pia huchangia baadhi ya dawa kubaki ghalani.

“Kuna wakati mahitaji hubadilika na kufanya baadhi ya bidhaa zisitumike kwa wingi kama ilivyotarajiwa,” amesema.

Ameongeza kuwa MSD imeboresha upatikanaji wa dawa za afya ya akili na iko mbioni kusambaza dawa ya kusaidia kuacha pombe, ambayo hapo awali ilikuwa ikipatikana zaidi katika sekta binafsi.

Naye Meneja wa Mawasiliano wa MSD, Etty Kusiluka, amesema malalamiko mengi ya uhaba wa dawa yanatokana na wananchi kwenda katika vituo visivyotoa huduma husika.

Meneja wa Mawasiliano wa MSD, Etty Kusiluka.

“Ni muhimu kuzingatia ngazi ya kituo. Dawa za msingi zinapaswa kupatikana zahanati, lakini si kila dawa inapatikana huko,” amesema.

MSD imesisitiza kuwa inaendelea kuboresha mifumo ya usambazaji na elimu kwa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma sahihi kwa wakati.